0

NI furaha iliyoje kukutana tena katika safu yetu nzuri ya kuelimishana juu ya mapenzi? Sina shaka utakuwa mzima wa afya njema na upo tayari kupata kitu kipya. Nakukaribisha kwa moyo mkunjufu tuongeze maarifa.

Rafiki zangu, leo nazungumza juu ya jambo muhimu sana katika mapenzi; uaminifu. Huu ndiyo msingi wa uhusiano, ndoa na mapenzi. Ikiwa uhusiano utakosa uaminifu, ni wazi kwamba hautakuwa na umri mrefu.


Uaminifu ni jambo lenye mvutano mkubwa, ni mjadala usiokwisha tangu kuwepo kwa mapenzi. Ukweli ni kwamba uaminifu ndiyo kipimo cha kwanza cha kugundua kama penzi lako ni la kweli au moyo wako unakudanganya.


Hata hivyo upo ukweli ambao hauwezi kukwepwa! Uaminifu unawashinda wengi sana walio kwenye uhusiano. Watu wanashindwa kuwa waaminifu kabisa. Pamoja na yote hayo, zipo sababu ambazo zinaelezwa zinasababisha mwenzi kukosa uaminifu kwa mpenzi wake.

Hebu twende tukaone ni kwa nini watu wanakosa uaminifu.

KUKULIA KATIKA IMANI...

Hili ni la kwanza kabisa ambalo unapaswa kulifahamu rafiki yangu mpenzi, malezi ya kiimani! Neno uaminifu tukilinyambua tunapata maneno imani, amini na aminiana. Kwa msingi huo basi, ikiwa mpenzi wako hajakulia katika mazingira mazuri ya kiimani kulingana na taratibu za dini anayoiamini ni vigumu sana kuwa mwamnifu au kukuamini!Hii ina maana kwamba wakati unachagua mchumba ni vizuri kuangalia pia suala la imani ya dini yake.

Je, ni muumini kikamilifu katika imani yake? Maana katika imani za dini, kitu cha kwanza kabisa kufundishwa na kutiliwa mkazo ni uaminifu! Katika uaminifu huwezi kukuta uongo, usaliti, masengenyo na mengine mengi ambayo siyo mema.

Mwaminifu ana hofu, atapenda kuzungumza ukweli siku zote maana imani ya dini yake inamsuta.

 UNAPASWA KUWA MWAMINIFU
Ikiwa ni kweli unahitaji kuwa na mwenza wa peke yako, basi lazima uanze kujiamini kwanza wewe mwenyewe. Hili ni jambo la kwanza kabisa kwako, ukikosa uaminifu basi ujue lazima mpenzi wako naye atakusaliti.

Jifunze kuwa mkweli siku zote, kila mmoja anajua jinsi gani ukweli unavyouma lakini unapomwambia mpenzi wako ukweli anajisikia furaha, huru na amani kuwa na wewe. Anajiona bora maana amepata mpenzi mkweli na muaminifu.


Hakuna haja ya kumdanganya mpenzi wako ulipotoka kazini ulipitia kwenye pati wakati ulikwenda kuangalia shoo kwenye kumbi za burudani.


Kumbuka kwamba unaweza kumdanganya na akakuamini lakini kumbe ukiwa huko kwenye starehe zako kuna mtu anayemfahamu mpenzi wako alikuona na akaenda kumwambia, unafikiri akikuambia ulionekana huko itakuwaje?


Lazima atahisi kuna kitu kingine unamficha ulichokuwa ukifanya huko, ingawa pengine hukuwa na kitu kibaya zaidi ya kuangalia shoo ya bendi uipendayo; sasa ili uweze kuzima hisia hizo ni vyema kuwa mkweli. Mweleze tu: “Samahani sweetie, unajua jana nilikuwa nimechoka sana, rafiki yangu akaniomba niongozane naye kwenye muziki, lakini naomba unisamehe sikuweza kukutaarifu mapema.”


Ni sentesi fupi inayoonyesha uungwana wa hali ya juu, uaminifu na kujali uwepo wa mpenzi wako. Hapa unamfanya ajisikie yeye ni maalum kwako.


NI MWAMINIFU KWAKO?

Katika ulimwengu wa mapenzi, hili ni jambo la msingi sana. Huna sababu ya kuwa na mpenzi asiye mwaminifu, sasa ili usije ukaingia katika mkumbo huu ni vizuri kumchunguza lahazizi wako kwa muda mrefu.

Mwekee mitego, chunguza kauli zake, kumbukumbu zake na mienendo yake, ana uaminifu kweli? Maana asiye mwaminifu hupoteza kumbukumbu juu ya mambo aliyoyafanya.


Hata kama unampenda kiasi gani lakini kama umegundua hana uaminifu ni vizuri kuachana naye mara moja. Mpenzi asiye mwaminifu wa kazi gani? Sana sana atakusababishia presha bure!


JIAMINISHE

Ikiwa ni kweli unampenda mpenzi wako kwa dhati basi inabidi ukubali kuwa katika himaya yake kiuaminifu. Hii ina maana kwamba, mwenzi wako ana uhuru wa kukuchunguza atakavyo ili aweze kuwa na amani ya moyo wake kwako.

Umpe uhuru wa kuishika simu yako na ikiwezekana kuikagua na kukuuliza maswali kuhusu chochote kilichomo katika simu yako. Kama ‘umesave’ picha ya mtu wako wa nje, akaiona na kukuuliza ni kwa nini unayo hiyo picha kwenye simu yako uwe na sababu za maana za kumweleza!

Huwezi kutaka uaminifu katika penzi lako kama wewe mwenyewe hutaki kuwa katika himaya ya uaminifu.

ANZA KUWA MWAMINIFU!

Ni kweli kwamba kipengele kilichopita ni kigumu sana hasa kwa wanaume wenzangu lakini kama ni kweli una mapenzi ya dhati kwa patina wako inakubidi ukubaliane nacho. Silaha pekee ya kuweza kuwa huru na kipengele hicho ni wewe mwenyewe kuwa MWAMINIFU.

Anza sasa kuwa mwaminifu na utafurahia mapenzi ya kweli kutoka kwa mpenzi wako. Inawezekana kuna vitu vingi ulikuwa ukivikosa kwa mpenzi wako, lakini kumbe tatizo lilikuwa dogo sana, uaminifu! Kwa nini uaminifu ukushinde? Inawezekana kama utauachia moyo wako kikamilifu kwa mwenzi wako. Chukua hatua

Post a Comment

Kama umependezwa na hii stori toa maoni yako kama unayo

 
Top