0
Rafiki zangu, kugombana hakuna maana ya kumalizika kwa uhusiano hasa kwa wale walio kwenye ndoa. Mambo yanatokea, yanatatuliwa na mwisho wake maisha yanaendelea kama kawaida.

Kwa bahati mbaya sana ni kwamba, wengine wanapokuwa kwenye migogoro na wenzi wao, badala ya kutafuta njia za utatuzi, wanazalisha tatizo lingine!
Jambo la kusikitisha ni kuwa, tatizo jipya linalozaliwa linaweza kusababisha matatizo makubwa zaidi katika uhusiano huo na mwisho wake kusababisha kuachana kabisa.
Ngoja tupanue mawazo yetu leo hapa kwenye All About Love. Zipo kauli ambazo ukizitoa kwa mpenzi/mke/mume wako wakati mkiwa kwenye ugomvi, zinaweza kuzalisha tatizo kubwa zaidi mbeleni.
Tutaona tu. Tuendelee kuwa pamoja.

KWA NINI KAULI?
Inawezekana ukajiuliza; ni kwa nini nimesema kauli? Rafiki zangu, kwa kawaida, watu wakiwa kwenye ugomvi, jambo kubwa linalotokea ni kutupiana maneno.
Katika hali hiyo basi, kwa wenzi au wanandoa ni vyema kuchunga ndimi zao maana zinaweza kusababisha matatizo makubwa siku zijazo. Sasa twende tukaone... 

‘HUNA AKILI’
Wako baadhi ya watu wakigombana (hasa wanaume) wamekuwa na tabia ya kuwaambia wanawake wao: “Wewe huna akili kabisa...yaani hutumii akili kabisa katika kufanya mambo yako.
“Unakurupuka tu. Sasa ishu kama hii, hata mtoto mdogo anajua ni makosa, inakuwaje wewe unakosea?”
 
Hili ni jeraha la moyo. Mwanamke ukimwambia hana akili anajisikia vibaya, unampa kovu kubwa moyoni mwake. Anajiona wa hali ya chini na anahisi ameshuka thamani yake.
Kwake, kumwambia hana akili, ataanza kuwaza kuwa yupo mwanamke mwingine ambaye kwako ana akili kuliko yeye. Ni maumivu makali sana kwake.

‘NITAKUACHA’
Baadhi ya wanaume wana ulemavu huu. Ugomvi kidogo tu, atamwambia mwenzake: “Endelea na tabia zako za hovyo, ipo siku utajuta. Nimevumilia mengi sana lakini kuna siku nitachoka.
“Hutaamini macho yako. Siyo lazima niishi na wewe. Siwezi kuendelea kuteseka nikiwa na wewe. Nitakuacha nakuambia ukweli.”
Hii ni kauli mbaya ambayo inapandikiza chuki ndani ya moyo wa mwanamke. Kwanza kwa kumwambia hivi, hata kama alikuwa hakusaliti, unamfanya aanze kufikiria kutafuta mtu mwingine wa kumliwaza.
 
Kauli hii hasa kama ukiirudia zaidi ya mara mbili, humkaa akilini mwake na huanza kuwaza kuhusu kuwa na mwanaume mwingine nje ili apate mahali ambapo hata kama ukimuacha, atapata pumziko la uhakika.

‘NAKUVUMILIA TU’
Ni kweli mapenzi ni uvumilivu. Kuvumiliana ni siri ya uhai wa ndoa nyingi lakini hilo linapaswa kubaki moyoni.
Kugombana na mwenzako halafu umwambie kuwa unamvumilia tu, inamaana kwamba kuna siku uvumilivu wako utaondoka na utafanya maamuzi magumu – kuachana!
Si kauli njema kwa mwenzi wako. Mbaya zaidi humfanya aanze kufanya maandalizi ya mtu wa kuziba nafasi yako hata kama ni kwa usaliti. 

‘KUNA SIKU UTAJUTA’
Kauli hii haina tofauti kubwa sana na iliyotangulia maana kinachofanyika hapa ni kumuandaa mwenzi wako kwa ajili ya matatizo siku zijazo.
Kumwambia: “Kuna siku utajuta, endelea na mambo yako tu, utaona.” Hii inamaanisha kwamba, uamuzi ulio ndani yako si mzuri kwake lakini ni suala la muda tu.
Ataamini (na ndivyo ilivyo mara nyingi) kuna muda ambao atajuta sana kwa sababu yako. 
Hiyo ni sawa na kutengeneza bomu unaloliandaa kulilipua muda ujao.
Bado zipo kauli zaidi ambazo zina maudhi lakini pia zinaweza kusababisha matatizo zaidi kwa mwenzi wako

Post a Comment

Kama umependezwa na hii stori toa maoni yako kama unayo

 
Top