Kila mmoja ana uhuru na haki ya kupenda. Huwezi kuchaguliwa wa kumpenda! Mapenzi ni maisha ya mtu katika uhalisia wake.
Hii humaanisha kuwa kama utakuwa na mtu ambaye moyo wako hauna mapendo ya dhati kwake, tafsiri yake ni kwamba, maisha yako yote yatakuwa yenye mateso kila siku.
Utalala na mtu usiyempenda, utaamka naye na utaambatana naye baadhi ya sehemu wakati moyo wako haukuwa tayari kuwa naye. Hilo ni tatizo. Kwa bahati mbaya kuna baadhi ya wazazi bado wana mawazo na fikra za kizamani.
Wapo wanaoendelea kuwachagulia au kuwalazimisha watoto wao wenzi wa kuishi nao. Ndugu zangu, hizo ni zama za kale. Maisha yamebadilika. Kila kitu kimebadilika. Ni sahihi zaidi mtu achague mwenzi wa maisha yake mwenyewe maana ataishi naye yeye na siyo mzazi au mwingine yeyote.
Huo ni upande mmoja; upande mwingine ni haki ya mwanamke kupenda. Imezoeleka mwanaume ndiye mwenye mamlaka ya kumpenda mwanamke na kumtaka waanzishe uhusiano.
Inategemea kama mwanamke atakubali au atakataa. Pengine ni utaratibu sahihi maana ni uamuzi wa mwanamke na kuangalia moyo wake kama ni kweli amempenda mwanaume huyo au lah kisha anaamua mwenyewe.
Kuna wakati mwanamke anazama katika mapenzi kwa mwanaume. Kila akipita mbele yake, moyo unalipuka. Kila anachokifanya anazuzuka. Mapenzi yamemwingia lakini sheria inambana. Hawezi kuanzisha uhusiano yeye.
Hata kama akiamua kujipeleka, mwisho wao hauwi mzuri – wataachana tu (mara nyingi). Tafiti zinaonyesha kuwa, uhusiano ulioanzishwa na mwanamke mara nyingi huwa hauna mafanikio kama unaoanzishwa na mwanaume.
Akili za wanaume wengi huamini mwanamke anapomfuata na kumtaka kimapenzi ni mhuni au kwa lugha za vijana anaonekana hajatulia! Si jambo sahihi, hutegemea na moyo wa mhusika na namna anavyoonesha mapenzi yake lakini ndivyo ilivyozoeleka.
Pamoja na hayo, mwanamke anaweza kumvutia mwanaume aliyempenda na kumuingiza kwenye himaya yake kwa kufuata utaratibu ulio sahihi na penzi likadumu.
Kwanza utajihakikishia kuwa huonekani mhuni na bado uhusiano wenu ukawa wenye nguvu, penzi la dhati na lenye kuvutia. Hakika inawezekana. Ni suala la kufuata tu utaratibu uliopendekezwa.
Hapa chini sasa nitakupa mbinu rahisi ambazo zinaweza kukusaidia kumnasa mwanaume anayeusumbua moyo wako. Kwa nini uteseke wakati njia za kumnasa zipo? Hebu twende tukajifunze...
MVUTO
Kwanza kabisa, kama mwanamke unapaswa kuwa katika mwonekano mzuri wa kike wenye kuvutia muda wote. Hapa nasema hivyo kwa sababu wapo wanawake ambao wanahangaika na hawajaolewa au hawajapata watu waliotangaza nia kwa sababu tu hawajiweki katika mwonekano mzuri.
Mwanamke jitambue. Tengeneza na hifadhi mvuto wako siku zote. Zingatia mavazi bora, yenye staha na kukusitiri.
Baadhi ya wanawake huamini katika mavazi yanayowaacha baadhi ya sehemu ya miili yao nje. Siyo sawa. Mwanamke staha. Anapaswa kujiheshimu na kujihifadhi.
Kujianika na kujiacha wazi, kutakufanya uonekane mhuni, usiye na maana na hivyo hata kama ukifanikiwa kumnasa, fahamu kuwa mwisho wenu utaishia kwenye mapenzi tu na siyo ndoa.
Ni vyema pia ukazingatia kuhusu mtindo wa nywele na vipodozi kulingana na mahali ulipo. Hili nitalifafanua vizuri kwenye vipengele vinavyofuata.
Huu ni mwanzo mzuri wa kuelekea kwenye kumnasa mwanaume anayeutesa moyo wako. Usijali, utatulia tu. Wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.
GPL
Post a Comment
Kama umependezwa na hii stori toa maoni yako kama unayo