Ni wiki nyingine tulivu kabisa tunakutana tena kupitia safu hii nikiamini umzima bukheri wa afya na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku kama kawaida.
Mimi
namshukuru Muumba wa mbingu na ardhi kwa kuniwezesha kutimiza majukumu
yangu ya kila siku likiwemo hili la kuelimishana na kukumbushana juu ya
mambo yanayogusa maisha yetu ya kimapenzi.
Mpenzi msomaji wangu,
wiki iliyopita nilikuwa na kazi kubwa ya kumshauri rafiki yangu ambaye
aliniletea mashitaka ya mpenzi wake kutembea na rafiki yake.
Nilipata wakati mgumu sana kwani nilipoongea na msichana akaniambia
wazi kwamba, amekuwa hapati penzi alilotarajia kutoka kwa rafiki yangu.
Msichana huyo akaenda mbele zaidi na kusema kwamba, yule shemeji yake
alionesha kumjali sana kiasi kwamba siku alipomtamkia kwamba anampenda
ilimuwia ngumu kukataa.
Kuna kitu cha kujifunza hapa kwamba endapo utaishi na mpenzi wako
bila kumdhihirishia kwamba unampenda kwa dhati, akitokea mtu wa pembeni
akaonyesha kuwa kafa kaoza, tarajia kusalitiwa kama siyo kuachwa kwenye
mataa.
Unapokuwa umeanzisha uhusiano na mtu, utambue ana watu wengi
wanaomtaka lakini huenda anawakatalia kwa kuwa yuko na wewe, sasa
ukionesha kutomjali, hawezi kuendelea kuwa muaminifu kwako. Atachepuka
na hata kama ataendelea kuwa na wewe ni kwa kuwa labda hana ujasiri wa
kukuacha.
Ndiyo maana leo nikaona nikupe sababu ambazo zinaweza kumfanya mpenzi
wako akatembea na rafiki yako tena wakati mwingine kwa siri bila wewe
kujua.
Wewe mwenyewe
Endapo utakuwa
umeanzisha uhusiano na mtu, wewe mwenyewe unaweza kutengeneza mazingira
ya kusalitiwa. Usipoonesha kumpenda, kumjali, kuthamini penzi lake kisha
rafiki yako akayaonesha hayo kwake, ni rahisi sana kukupiku.
Kwa mfano, endapo umekuwa na mpenzi wako lakini hata siku moja
hujawahi kumpa zawadi au kumtoa ‘out’, siku shemeji yake (rafiki yako)
akiamua kufanya hivyo, mpenzi wako atahisi yeye ni mtu sahihi kwake.
Kujirahisi kwake
Wapo ambao wanatembea na mashemeji zao kwa sababu tu ya kujirahisi
kwao. Kwa mfano unapopendelea kuzungumza mambo ya chumbani na rafiki wa
mpenzi wako unatarajia nini? Unapomvalia kihasara rafiki wa mpenzi wako
lengo linakuwa ni lipi?
Mbaya zaidi ni pale utakapokuwa na mashemeji
ambao hawabipiwi. Hapa namaanisha wale ambao wakiona dalili ya kupendwa
tu, wanaomba chansi.
Haishauriwi kumuamini sana rafiki yako kwani wengine wakipewa uhuru wa
kuwa karibu na mashemeji zao, huchukulia kama fursa ya pekee.
Kwa mfano, unapomuamini rafiki yako kiasi cha kumruhusu aende na mpenzi wako baa, klabu au ufukweni ni kujitafutia matatizo.
Tunajua kwamba wapo marafiki waaminifu lakini tambua tu kwamba wengi
wanapokuwa katika mazingira hayo ndipo huishia kusaliti na wakati
mwingine bila kupenda.
Kwa nini nasema bila kupenda? Chukulia
umemruhusu mpenzi wako aende baa na rafiki yako, wamekunywa pombe hadi
wamelewa kisha rafiki yako anamchukuwa mpenzi wako kwenye gari
kumrudisha nyumbani.
Wengi kwenye mazingira hayo uzalendo unawashinda. Kwa hiyo kama
hutaki yakukute ya kusalitiwa, kama una tabia ya kumruhusu mpenzi wako
kwenda baa na shemeji yake, acha mara moja.
Rafiki mnafiki
Unaweza kuwa na rafiki lakini
kumbe ni mnafiki. Huyu ni yule ambaye mko pamoja lakini anajiapiza
kwamba siku moja lazima atakuchukulia mpenzi wako. Huyu ndiye tunamuita
rafiki mnafiki.
Kutokana na tabia hizo ndiyo maana matukio ya baadhi ya wanaume
kuwatongoza wapenzi wa marafiki zao yamekuwa yakiongezeka. Pia wanawake
wengi sasa hivi hawaoni hatari kuwatongoza marafiki wa wapenzi wao au
wapenzi wa mashoga zao.
Penzi la kweli
Mfano Juma ana mpenzi wake
aitwaye Asha na Juma ana rafiki yake aitwaye Jamali. Juma na Asha ni
wapenzi lakini hawapendani kivile ila Jamali anaonekana kuwa na penzi la
kweli na Asha na wakati huohuo Asha naye anahisi kuwa na penzi la kweli
na Jamali.
Katika mazingira hayo usije ukashangaa siku moja kusikia Asha
katembea na Jamali. Siyo kutokana na tamaa au ushawishi bali ni kutokana
na uwepo wa penzi la dhati kati yao.
Katika mazingira haya ndipo
ambapo tumekuwa tukisikia fulani kamuacha mkewe kisha yule mke kaolewa
na mwanaume ambaye alikuwa rafiki wa wanandoa hao.
Tamaa tu
Endapo utagundua mpenzi wako katembea
na rafiki yako, kuna uwezekano ameshawishiwa kwa pesa au mali. Hii ni
kwa sababu wapo watu ni dhaifu sana, yaani wao kusaliti wapenzi wao kwa
sababu ya pesa, mali au tamaa zao za kimwili siyo kitu kigumu.
Ndiyo maana tunashauriwa kuwa na wapenzi ambao hawana tamaa za
kijinga. Katika siku za mwanzo za uhusiano wenu ukigundua uliyenaye si
mtu wa kuridhika na penzi unalompa, pesa na mali mlizonazo, mapema
muonyeshe mlango wa kutokea kwani itakuwa siyo jambo la ajabu kusikia
katembea hata na ndugu au rafiki yako.
Post a Comment
Kama umependezwa na hii stori toa maoni yako kama unayo