0

NI siku nyingine tunakutana tena kwenye safu yetu nzuri ya Love & Life. Lengo ni lilelile, kupeana mawili matatu kuhusu maisha yetu ya kimapenzi.Kila siku tunapaswa kujifunza zaidi kuhusu uhusiano na mapenzi maana maisha yetu hatuwezi kuwakwepa wenzi wetu hivyo ni vyema kujua mbinu mpya kila wakati za kuwafanya wenzetu wafurahie uwepo wetu.

Nimekuwa nikisisitiza mara kwa mara, usimwonyeshe mpenzi wako kuwa hana thamani. Mpe nafasi akueleze hisia zake. Kumsikiliza na kujua kilicho moyoni mwake kutakurahisishia kuishi naye kwa furaha maana utakuwa unafanya mambo ambayo yanampendeza.

Rafiki zangu, sasa tuendelee na mada yetu ambayo ilianza wiki iliyopita. Nilifafanua mambo mengi ambayo ni muhimu sana kwa wapenzi. Unajua kuna vitu ambavyo wengine wanaweza kuvidharau na kuviona vya kawaida lakini kumbe vina thamani kubwa sana.

Mfano wanawake wengi huwa bize kuhakikisha wanaume wao wanakuwa wenye furaha na wanajiona wapo peke yao kwenye uhusiano. Ni jambo zuri, lakini kwa wanaume ni tofauti kabisa.
Hawana muda wa kuangalia mambo ambayo yanaweza kuwa kivutio kwa wenzi wao. Hilo ni tatizo kubwa sana kwenye uhusiano. Kwa bahati nzuri ni kwamba, wanawake huwa wanafurahishwa na mambo madogo sana.

Wanapagawishwa na vitu vya kawaida sana ambavyo vipo ndani ya uwezo wa mwanaume. Hebu twende tukaone vitu vingine ambavyo huwachanganya wanawake.

UJUMBE WA MAHABA
Kumtumia mpenzi wako au mkeo ujumbe wa mahaba ni sehemu ya kumwongezea ‘uchizi’ katika penzi lenu. Wengi hawapendi na pengine hawawezi kutunga meseji za kimahaba.
Kwa bahati nzuri ni kwamba, siku hizi za utandawazi mambo ni rahisi sana, magazeti mengi yanaandika Love Messages – za Kiingereza na Kiswahili.

Achana na magazeti hata baadhi ya kampuni za simu hufanya hivyo. Kwa gharama ndogo unaweza kujiunga na huduma hiyo kisha ukawa unatumiwa meseji kila siku.

Mitandao mbalimbali ya kwenye kompyuta nayo huandika meseji mbalimbali. Kitu cha kufanya hapo ni kukopi kisha kurekebisha kidogo kama utaona kuna vitu vya kuboresha kidogo, kisha mtumie mpenzi wako.

Unaweza kuona ni kitu kidogo sana, lakini utaona atakavyozidi kukupaisha kithamani katika maisha yake. Kama ulikuwa hujawahi kufanya, hebu anza utaona faida yake.
Fanya hivyo kulingana na nyakati, mfano asubuhi njema, mlo mwema, usiku mwema nk. Ni utaratibu mzuri sana kimapenzi.

MITANDAO YA KIJAMII
Siku hizi kuna mitandao mingi ya kijamii. Kwa bahati mbaya, baadhi ya watu huitumia vibaya na kuanzisha uhusiano usiofaa huko. Wanawake wengi huwa hawana amani na wanaume zao hata kama kwenye maelezo yao ya utambulisho wameandika wameoa au wana wachumba.

Kuweka picha yake mara chache au maneno ya kuonyesha unavyompenda, huziba hisia zake mbaya na kujiona yuko na mwanaume huru na makini.

Lakini hata hivyo, utakuwa umejiwekea ulinzi madhubuti na kuwafanya wanaofikiria kuwa na wewe wabadili mawazo yao wakijua kuwa nafasi imejaa! Jaribu utaona ukweli wa ninachokisema.

KUWA HURU NAYE
Wanaume wengi hawapendi mahaba, lakini asikudanganye mtu, kuongozana na mwenzi wako huongeza msisimko na kumfanya azidi kuwa huru na mwenye kujiamini. Usimwogope, mshike mkono, tembeeni huku mnamzungumza.

Kichwani hujiona mwanamke kamili, aliye na mwanaume asiye na ‘vimeo’ mitaani. Haya ni machache kati ya mengi ambayo kwa hakika hustawisha penzi.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa. 

Post a Comment

Kama umependezwa na hii stori toa maoni yako kama unayo

 
Top