0


UHUSIANO  wenye amani na masikilizano ndiyo kitu ambacho kila mmoja wetu anakihitaji na ikiwa hivyo unaweza ukajikuta unanawiri tu!  

Wakati mwingine unaweza hata kujikuta hujala chochote lakini ukajihisi umeshiba eti kwa sababu tu umemuona mpenzio au kuwa naye karibu tu, yaani yeye kwako ndiyo mambo yote, yeye ndiyo kila kitu kwenye maisha yako! Huo ndiyo utamu wa maisha!

 
Naamini kabisa wapo ambao wako katika aina hiyo ya mapenzi na hao wanatakiwa kumshukuru Mungu kwa kuwaweka kwenye mazingira hayo.
 
Lakini sasa wakati wengine wakiishi kwa raha katika maisha yao ya kimapenzi, wapo wengine wanaoishi na wapenzi wao huku mioyo yao ikiwa imesinyaa, yaani hawana furaha kabisa! 
 
Kwao kila siku ni karaha na vituko vya makusudi kutoka kwa wapenzi wao licha ya kwamba wanawapenda sana na kuonesha mapenzi yao yote. 
 
Cha ajabu sasa, licha ya baadhi ya watu kutokuwa na furaha katika maisha yao ya kimapenzi eti wanahisi njia sahihi ni kuvumilia huku wakiamini siku moja mambo yatabadilika.
Jamani, huenda nikawa na msimamo tofauti kidogo kwani mimi naamini mapenzi ya kweli ni pamoja na kumsikiliza mwenzio na kuheshimu hisia zake, hasa kwenye mambo yanayofaa.  

Tofauti na hapo, tabia ya kutokuwa msikivu, kutojali na kutokuwa mwepesi kubadilika ni dalili tosha ya kutokuwepo kwa upendo wa dhati.  Mapenzi, nijuavyo mimi ni kupenda, 
kupendwa, kusikilizana, kupatilizwa na kuheshimiana na si kinyume chake!
 
Wakati mwingine unaweza kujikuta katika wakati mgumu wa kuamua hatima ya uhusiano wako na mpenzio kwa kuwa unahisi unampenda sana na kwamba hauko tayari kumkosa. 
 
Ukweli ni kwamba, hata kama huyo uliyenaye unampenda vipi lakini kama anaonesha kubadilika na kutokupa ile furaha uliyotarajia, huna sababu ya kumng’ang’ania. Muache aende zake kwani huenda kuendelea kuwa naye ndiyo kuyafupisha maisha yako.
 
Inawezekana kuna mambo mazuri ambayo amekuwa akikufanyia huko nyuma kiasi kwamba ukikumbuka unasita kufanya maamuzi ya kumtosa. Sikiliza nikuambie kitu, unapokutana na hali hiyo elewa ni shetani ambaye anataka kukufanya uendelee kuwa kwenye utumwa wa mapenzi.
 
Pata ujasiri, yaliyopita katika uhusiano wako, yafanye kuwa historia kisha fanya uamuzi sahihi. Uamuzi sahihi ni upi? Sidhani kama hapa panahitaji darasa zito. 
Uamuzi wa kwanza ni kukubali kuendelea kuwa kwenye uhusiano huo. Utaamua hivyo kama utaona kwamba uko tayari mapenzi yakuue lakini siyo kumuacha huyo uliyetokea kumpenda. Ila kumbuka wanaochukua uamuzi huu ni malimbukeni wasiyoyathamini maisha yao.
 
Uamuzi mwingine ambao naona ni sahihi ni ule wa kumuacha aende kisha wewe uyaache maisha yako yaendelee kuwepo. 
Amini bila kuwa naye bado maisha yako yanaweza kuendelea kuwa ya furaha na wala huwezi kujuta. Utajutaje wakati alikuwa akikunyima furaha uliyoitarajia?

Post a Comment

Kama umependezwa na hii stori toa maoni yako kama unayo

 
Top