0

MNAMO miaka mitatu iliyopita, nikiwa nimemaliza shahada yangu ya kwanza ya ualimu. Nilibahatika kukutana na msichana ambaye sijui nimwelezee vipi ili utambue kuwa alinivutia.

Tabia zake tangu aliponipisha kiti niketi ndani ya daladala baada tu ya kutambua kuwa mimi ni mrefu sana hivyo naumia sana kuinama katika daladala ile.

Msichana wa mjini kumpisha kiti kijana mwenzake ndani ya daladala? Ilinistaajabisha. Ningekosa ustaarabu iwapo nisingetoa shukrani kwa mwanadada yule, na hapo ukaribu wetu ukaanzia. Akanipa namba yake ya simu bila kusita. Akanieleza kuwa anakaa Gongo La mboto nami nikamweleza kuwa ni mwenyeji wa Dar lakini nipo Mombasa kikazi na nd’o kwanza nimepata ajira.



Bahati nzuri aliwahi kufika Mombasa pia, hilo jambo likatuweka karibu zaidi. Hata nilipofika nyumbani na kuwasimulia watu wakanieleza kuwa huenda ni bahati yangu na huyo ni mke ameletwa katika namna ya maajabu.

Mawazo ya marafiki yakanisukumu kumpigia simu!!! Kitu cha kwanza nikamuuliza anaitwa nani? Badala ya kujibu akakata simu, nikaduwaa lakini baada ya dakika tano akanipigia na kulalamika kuwa kuna jambo alikuwa anafanya hivyo asingeweza kuongea ndo maana akakata.


 Sasa tuliweza kuzungumza akanieleza kuwa yeye anaitwa Ulfat Mustafa. Nikafarijika kutambua kuwa alikuwa dini sawa na mimi hivyo kama ni kweli angefaa kuolewa basi pasingekuwa na mtafaruku wowote.
 Nami nikamweleza kuwa naitwa Salim Ally. Tukabadilishana mawazo kwa muda mrefu, na kuanzia siku hiyo tukawa tunawasiliana kwa meseji ama kupigiana simu. 

 Ukaribu hukuza mahusiano, hali ya kujali huzua mapenzi yasiyotarajiwa. Ulfat alikuwa ananijali sana, nami nikalipiza kujali huko. Hapo zikaibuka hisia fulani za ajabu kwangu, nikaanza kuwa nakosa raha yakipita masaa mengi bila kuzungumza na Ulfati. Nikaanza kuwa na wivu nikipiga simu ya Ulfat usiku na kukuta anazungumza na mtu mwingine.

 Na hapo nikajagundua kuwa tayari nilikuwa penzini!! Nikaona si haki kuinyima nafsi yangu haki. Nikaamua kumtafuta Ulfat tukaketi katika fukwe za koko, nikamweleza yangu ya moyoni. Ilikuwa kama bahati, japo Ulfat alipinga kwa nguvu hoja hiyo baadaye alinikubalia. Tukakumbatiana.

 Baada ya juma moja tukaenda kupima virusi. Hakuna aliyekuwa ameathirika. Tukataka kufanya mapenzi kwa mara ya kwanza lakini kila mmoja akaja kushtuka kuwa siku inayofuata ilikuwa ni siku ya kuanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. 

Hatukuwa tayari kujitia najisi kubwa kiasi kile. Tukakubaliana kuwa tuwe wavumilivu tena wacha Mungu sana hadi hapo tutakapobarikiwa.

 Hatukutaka kuonana maana tungetiana majaribuni, na simu za mara kwa mara zikapungua maana kila tulivyozungumza kwa muda mrefu nilijikuta nashawishika kimahaba!!! Umbali kati yetu ukatusahidia kwenda sawa kuanzia chungu cha kwanza hadi kile cha mwisho katika mfungo!! Nilitambua vyema kuwa nahitajika kazini siku mbili tu baada ya mfungo kumalizika.

 Marafiki niliowaamini wakaniambia ili Ulfati anikumbuke sana na kunipenda kwa dhati natakiwa kufanya naye mapenzi kwanza. Wakaenda mbali zaidi na kusema kuwa nikimwacha hivi hivi wajanja watamchukua na mwishowe nitaula wa chuya.

 Mwanzoni maneno yao hayakuniingia lakini hatimaye nikashawishika. Nakiri kuwa funga yangu ilikuwa batili maana nilihesabia siku zimalizike ili niwe huru na Ulfat wangu na kutimiza ushauri wa marafiki.

 Hayawihayawi hatimaye yakawa!! Usiku wa sikukuu ya IDDI nikapanga kukutana na Ulfat wangu. Sikumwambia lengo langu lakini tulikutana faragha mahali fulani, nikadhani na yeye ana hisia kama zangu na ananiamini sana. Hakupinga!!! Tukakutana katika sikukuu ya IDDI. Sikumweleza nia yangu lakini, kimatendo alijua kuwa nahitaji mahaba!! Alitaka kukataa lakini nikamshawishi zaidi akajiingiza mkenge!! Nikafumba macho huku nikijihalalishia kuwa nifanyalo ni sahihi.

 Tukakesha humo tukizungumza kimatendo MAHABA……. Asubuhi nikaamkia nyumbani kujiandaa kwa ajili ya safari ya kuelekea Mombasa. Ulfat alidai kuwa amechoka sana hataweza kunisindikiza. Nikamtumia pesa ya matumizi na kumwambia kuwa nitakuja tena nikipata nafasi ama yeye akipata nafasi.

MIEZI MITATU MBELE Kama ilivyokawaida yangu huwa ninamtindo wa kupima afya yangu!! Sikuwa na mashaka yoyote, nikaenda kupima bila kutarajia nikaambiwa kuwa mimi ni MUATHIRIKA. 


Nilipima tena na tena na majibu yakabaki kuwa vilevile, nilikuwa nina uhakika kuwa nilishiriki na Ulfati pekee tendo hilo baada ya kupima. Nikampigia simu Ulfati mida ya usiku nikamweleza juu ya utata huo. “Duh!! Yaani kumbe tangu siku ile nd’o leo umeenda kupima Salim.

 Pole sana jamani, yaani kati ya wote wewe ndo umechelewa kabisa kujitambua!!” alinijibu bila wasiwasi, nikamuuliza anamaanisha nini. “Salim eeh yaani wewe na akili zako timamu ukaona kabisa mimi ni msichana wa kuoa, Salim nimelaaniwa mimi na kizazi changu, natafuta wenzangu wa kulaaniwa nao. Huna haya Salim, na elimu yako kabisa na kujifanya mcha Mungu unatoka katika mfungo ambao nilidhani utakupa mwanga wa kunijua mimi vizuri kumbe hakuna ulichofunga Salim.

 Ukashindwa kujua kuwa umekutana nami ili nikuue….. tamaa zako zimekuponza hayawani mkubwa!! Upeo wako mkubwa lakini umekuwa dhaifu, hujui nani shetani na nani mtu safi.

 Unabambikiwa daktari wa kuchonga unajisifu kuwa tulipima Ukimwi wote….. ulipima mwenyewe Salim yule daktari nilikuchongea tu!!! Kajifie huko Salim, kafe kabisa na usikumbuke kuwa uliwahi kukutana na mtu kama mimi, maana nitakuwa nimetingwa na watu wengine wajinga wajinga kama wewe” akamaliza na kukata simu palepale. 

Nilikuwa natetemeka na kisha nikagundua kuwa nilikuwa najikojolea!! Sikuamini hata kidogo kama yule ni Ulfat anayesema nami vile.

 Nilikaa kitako nikajaribu kupiga namba yake, lakini haikupatikana tena!! Haikupatikana hadi muda huu ninavyuokuandikia haya…… 

Nimekuandikia haya siku hii ya leo. Kama ulipanga kuasi kama mimi, GHAIRI SASA….. Mimi yalinikuta!! Yalinikuta kwa sababnu ya uasi wangu na sijui kama nilisamehewa!!!!

NITAKUFA NIKIWA NAJUTA!! NISAMEHE DUNIA

*UJUMBE. Si kila king’aacho ni dhahabu….USIAMINI KWA KUPIMA KWA MACHO!!! **TAMAA zetu ndo zinatuhukumu katika kila Nyanja……IPINGE TAMAA ya mwili……UONGOZE MWILI WAKO.

***RAFIKI MWEMA hushauri mambo mema…..kuwa makini uchaguapo RAFIKI WA KUKUSHAURI nawe ukatumia vyema ushauri wake….Kumbuka si kila USHAURI ni USHAURI MZURI!!!

MWISHO

Post a Comment

Kama umependezwa na hii stori toa maoni yako kama unayo

 
Top