Nina wajibu wa kumshukuru Mungu wangu siku zote kutokana na uongozi wake imara katika maisha yangu. Yeye ndiye anayenitia nguvu na kunifanya niwe kama nilivyo. Ahsante sana Mungu wangu!

Mpenzi msomaji wangu, ikiwa huna kawaida ya kumshukuru Mungu, anza leo hii na faida zake utaziona. Hata katika uhusiano wako, unapomtanguliza Mungu katika kila kitu, atakuongoza na kukufanya mwenye furaha siku zote. Hii si simulizi ya kusisimua ya kitabu ni ukweli ambao upo wazi na kama ukichukua hatua utauona.

Katika uhusiano na mapenzi umakini wa hali ya juu sana huhitajika ili uweze kuwa bora kila siku na kuufanya uhusiano wako kuwa wenye nguvu na usiotetereka! Katika hili hutegemea zaidi jinsi unavyoendesha uhusiano wako.

Ukitaka mpenzi wako akuchoke au umchoke, wewe ndiye mwamuzi, lakini pia ukitaka mpenzi wako asikuchoke au usimchoke wewe ndiye mwenye uamuzi kwa kuwa una uwezo wa kuyafanya yote hayo. 

Wengi wanakuwa hawaelewi kuhusu hili, anaingia kwenye ndoa na mke wake au mumewe lakini baada ya muda anajikuta mapenzi yakipungua siku hadi siku mpaka anafikia hatua ya kuwa na mwanaume mwingine nje ya ndoa yake au kama ni mwanaume anaamua kuwa na nyumba ndogo! Hayo yote nayaita ni mambo ya kujitakia!

Inawezekana ukaendelea kuwa bora kwa mpenzi wako, inawezekana mpenzi wako akaendelea kuwa bora kwako ikiwa utahitaji kufanya hayo kwa dhati. Hakika kama ukitaka unaweza kuendelea kuwa wa kisasa katika uhusiano wako. Yapo mambo mengi sana ya kufanya ili uhusiano wako usitetereke. 

Katika mada hii nimekuandalia mambo 10 muhimu ambayo ukiyazingatia kwa umakini mkubwa uhusiano wako utakuwa imara siku zote. Kwa ufafanuzi zaidi, hebu fuatana nami katika vipengele vifuatavyo, naamini utaingiza kitu kipya ubongoni mwako.

MWANZO WA PENZI LENU!
Siku zote nimekuwa nikisisitiza kuwa, jinsi unavyoanza ndivyo utakavyomaliza! Waswahili hawakuishia hapo, wakaongeza kuwa; ‘Unavuna kile ulichopanda!’. Naamini katika semi hizo kuna mambo umejifunza. Kama ulianza vibaya uhusiano wako tegemea kumaliza vibaya, lakini kama ulinza vizuri basi tarajia maisha mazuri ya kimapenzi yasiyo na maumivu katika moyo wako.

Kama unatarajia kuingia katika uhusiano na mpenzi mpya hakikisha hujionyeshi tofauti na hali yako halisi ilivyo! Jifunze kujikubali, hata kama unafanya kazi ambayo unadhani ni hadhi ya chini, mbainishe mpenzi wako hali halisi ilivyo. Kama anakupenda, kazi yako haiwezi kupunguza mapenzi baina yenu.

Ikiwa ndiyo kwanza mnaanza uhusiano, zingatia hili, na kama mpo katika uhsiano kwa muda mrefu ukagundua wazi kuwa kuna mahali ulikosea, anza kufanya mabadiliko kuanzia sasa. Bado hujachelewa ndugu yangu.
Kudanganya hakuna mantiki, kudanganya ni utumwa, usikubali kuingia katika utumwa au kifungo cha aina hiyo. Ngoja niwape kisa cha rafiki yangu mmoja; jamaa alimdanganya mpenzi wake anafanya kazi katika shirika fulani kama kiongozi, akamwongopea kuwa mshahara wake ni mkubwa na mambo mengine mengi!

Yote hayo ilikuwa ni kumfanya mpenzi wake amuamini na kumpenda, akilini mwake akiamini pesa ndiyo mhimili wa mapenzi.
Kwa kuwa mpenzi wake alijua bioyfriend wake ana kazi na mshahara mzuri, alikuwa akimsumbua jamaa kila kukicha akafanyiwe shopping! Kilichotokea hapo ni kwamba jamaa alikuwa akimkwepa kila kukicha. Unajua kwanini alikuwa akimkwepa? Sababu ya pesa! Kama asingesema uwongo usumbufu wote alioupata asingeupata.

Jifunze kujikubali ulivyo, usitake kujionyesha kwa watu upo katika hadhi fulani wakati hali halisi haipo hivyo, huo ni ulimbukeni ambao unatakiwa kuushinda! Ukweli ni silaha ya kwanza katika mapenzi, anza hivyo kuanzia mwanzo na kama ulikosea, ulijisahau au hukujua, basi anza leo!
JIPENDE NA KUJITHAMINI...
Itakuwa kichekesho kama utasema unampenda mpenzi wako wakati wewe mwenyewe hujipendi! Huwezi ukasema unamthamini mpenzi wako wakati thamani yako mwenyewe huitambui.
Naamini tunakwenda sawa, kama unashindwa hata kuoga na kubadilisha nguo safi nani atakayekupenda? Huwezi kuwa wa kisasa kama huzingatii usafi, hakuna atakayevutiwa na wewe kama wewe hutaki kujivutisha. Sio ajabu mpenzi wako akakutosa kwa sababu tu huna muonekanano mzuri kwa rafiki zake.

Nani atakayekupenda wakati wewe mwenyewe huonyeshi kama unajitambua? Utakuta mwingine anajichukia bila mwenyewe kujua anajichukia! Unaweza ukamkuta mtu anajitoa kasoro mwenyewe, mara mimi mweusi sana mara mimi mweupe sana, miguu yangu imekaa upande, kwa nini nisingezaliwa kama fulani na maneno mengine yanayofanana na hayo. Amini ulivyoumbwa hakuna makosa yoyote, jinsi ulivyoumbwa unapaswa kuwa kama ulivyo.

Jikubali, jithamini! Kuwa msafi wakati wote, kauli zako ziwe safi siku zote mpenzi wako atakuwa huru kuwa na wewe. Isifikie hatua mpenzi wako akataka kutoka na wewe lakini akasita kwasababu hajui ukija utakuwa umevaa nguo za namna gani. Upo hapo?
 
Top