Mpenzi wako anayekupenda na kukuamini kupita kiasi, siku ukimtenda ndivyo sivyo, atakaa na maswali mengi kwa muda mrefu. Utageuka kinyaa mbele yake, kwa hiyo hata kukusamehe atapenda kufanya hivyo lakini atachelewa kwa sababu heshima yako kwake, imeondoka kabisa.
 
Pili; mapenzi yenu ni kama mnalazimisha. Hampendani kabisa au yeye hakutaki, kwa hiyo anaona hiyo ni fursa ya kukuadhibu. Utashangaa umemkosea jambo dogo lakini anavyolisimamia utadhani umeua mtu. Kama sura ya aina hiyo inajiri kwenye uhusiano wenu, jaribu kutazama mbele kwa matumaini. Hakupendi, atakupotezea muda.
 
Tatu; mapenzi yake kwako ni ya wastani. Ulivyo kwake, ukiwa naye ni sawa na hata usipokuwa naye, ni sawa vilevile. Huyu atakwambia anakupenda muda mwingine kwa sababu anachukulia ni kauli ya mazoea. Ila ukiyatafsiri mapenzi katika kipengele cha mguso wa moyo. Hakupendi, ila amekuzoea.
 
Kwa mtu wa aina hiyo, mlipaswa kuwa marafiki lakini mkajidanganya mkawa wapenzi. Hizo ni gharama za kulazimisha uhusiano. Elewa kwamba wapo watu ambao inatakiwa uwe na urafiki nao wa kawaida, halafu yupo mmoja ambaye ndiye mwenye nafasi yake. Anza kufanya upembuzi leo.
 
Mapenzi si kumuona mtu barabarani akakuvutia basi ukajiaminisha kuwa huyo anakufaa. Mwenzi wa maisha yako ni lazima akidhi vigezo vingi. Wapo ambao utalazimika kuwaacha barabarani wakirandaranda na dunia, halafu yupo mmoja mahususi anayefaa kwa hali zote kuwa mwandani wako.
 
Mada hii ikupe tafsiri kwamba siku za mwanzoni za uhusiano wako, inafaa utulize kichwa, ujadili mwenendo wa mwenzi wako kama anakufaa au la! Uzuri wa umbo na sura yake, visikufanye uwe kipofu ukasahau kilicho na faida kwa maisha yako ya leo na kesho. Tazama faida zaidi.
 
Unapoangalia tafsiri ya mwenzi wa maisha yako katika kipengele cha bahati, ni vizuri ukaweka kando hisia za kuridhishwa kitandani. Ufundi wake wa kukufanya usahau matatizo yako yote pindi mnapokutana faragha, si lolote endapo hatakuwa na sifa za kutimiza matarajio yako ya kimaisha.
 
Mwenzi wa maisha yako haendani na harufu yake. Kwamba ukiwa naye unajisikia mtulivu kiasi gani, la hasha! Kinachobeba uzito ni kiasi gani huyo uliyenaye anavyokupunguzia mzigo wa maisha yako. Je, mtindo wa maisha yake, haukupi mzigo wa moyo? Kama jibu ni ndiyo, basi iwe heri.
 
Wengine hutafsiri kwamba mwenzi wa maisha yako utamtambua kwa namna ambavyo anakufanya ujisikie hamu ya tendo mara kwa mara hata baada ya kutoka naye faragha muda mfupi uliopita. Mtazamo huu nao ni potofu, badala yake jiulize tena, je, mwenzi wako anakufanya ujihisi mtulivu?
 
Je, anakufanya ujione ni mwenye furaha? Nazungumzia furaha ambayo inakuja yenyewe, siyo ile ya kulazimisha. Mwenzi sahihi kwako kwa zaidi ya asilimia 99, anapaswa kuongeza kitu chanya kwenye maisha yako. Endapo ukijitazama unajikuta unazidi kupotea badala ya kusafiri kwenye mstari ulionyooka, hapo unazidi kupotea.
 
Yatazame maisha yako kabla hujakutana naye, halafu jiulize mabadiliko yako. Je, ni hasi au chanya? Inawezekana kweli ameyafanya maisha yako kuwa na furaha lakini hiyo furaha anaidumisha vipi? Isije ikawa anakufurahisha pale tu anapokuwa na shida zake, pindi unapomtatulia huyo anakwenda zake.
 
Top