ASILIMIA sabini ya wanaonipigia simu wakiomba ushauri baada ya kusoma mada zangu magazetini, hulalamikia kuhusu kuteswa na wapenzi wao. Kitu cha kushangaza zaidi ni kwamba, kati yao, asilimia themanini huwa wanaumizwa na wapenzi ambao wanawapenda sana.

Niweke sawa kidogo hilo, yaani wanakuwa na wapenzi ambao wao wanawapenda kwa mioyo yao yote, lakini ndiyo wanatesa kwa mambo mbalimbali. Kila akifikiria kuachana naye, anakutana na ukuta wa mapenzi ya dhati!

Hao ndiyo ninaowazungumzia hapa. Aidha wapo wale ambao wanaumizwa lakini hawajui kama wanaumia, lakini pia kuna wanaomia lakini wanaendelea kuvumilia wakiamini hawana ‘option’ nyingine, yaani kwa wapenzi wao wamefika na hata wakiachana inakuwa vigumu kupata mwingine!

Hizi ni fikra potofu sana. Ndugu zangu, katika mapenzi neno MATESO, MANYANYASO, KUSIMANGWA hayakubaliki kabisa. Hebu nitoe mfano mmoja, juzi nilizungumza na dada mmoja ofisini kwangu, akajaribu kueleza matatizo anayokabiliana nayo katika uhusiano wake. Ni binti mwenye umri wa miaka 28, ana mtoto mmoja ambaye baba yake alimkana!

Anaishi kwa taabu kwasababu hana kazi, kila siku amekuwa akianzisha uhusiano na wanaume lakini wamemtumia na kumuacha! Ni mwanamke mzuri kwa kumtazama, anavutia na anaweza kumshawishi mwanaume yeyote aliye mkamilifu lakini changamoto anazokutana nazo ndiyo hizo!

Ameshalia mpaka machozi yamekauka, mwisho akafikiri huenda amelogwa! Lakini mwisho wa siku nilizungumza naye na aliondoka akitabasamu, badala ya machozi aliyokuja nayo! Alikuwa na mwanaye anayeitwa James (5), mwenye afya nzuri na mchangamfu sana. Sitapenda kutaja jina lake, lakini alichovuna kwangu anajua mwenyewe!

Msomaji wangu, inawezekana kabisa na wewe upo katika mateso kama ya dada yetu huyo na hujui njia ya kutokea, usijali. Mimi nakuambia futa machozi yako. Inawezekana kabisa, kuna mahali ulipokosea katika maisha yako ndiyo maana leo hii mapenzi kwako yamekuwa mateso, lakini hiyo isiyo sababu!

Bado unayo nafasi ya kujipanga na kuanza upya kufurahia mapenzi. Kila kitu kinawezekana rafiki yangu.
Lakini lazima tukubali kwamba, wakati mwingine mapenzi ni mateso, ni chanzo cha kuingia kwenye matatizo maishani mwako.

Ndiyo maana Wataalamu wa Saikolojia ya Mapenzi wanasema ukikosea kuchagua mke/mume, basi tarajia maisha mabaya siku zote. Hii ndiyo kusema kwamba, mwanzo wa mafanikio bora maishani ni kuwa na mwenzi sahihi.

Unayempenda, anayekupenda na unayefurahia kuwa naye. Wanasaikolojia ya Mapenzi wanakubaliana moja kwa moja na hoja hii. Kwamba wakati mwingine mapenzi yanaweza kuwa chanzo cha mateso katika maisha ya binadamu. 

Kauli hii inashibishwa na hoja kwamba, mateso hayo yatasababisha na jinsi wewe mwenyewe utakavyokuwa umeingia na unavyoendesha uhusiano wako.

KWANINI MATESO?
Wapo ambao wanashangaa hoja hii, wanashangaa kwasababu tangu wamefahamu mambo ya mapenzi hawajawahi kuwa na uhusiano zaidi ya mpenzi mmoja ambaye pengine hivi sasa wapo katika ndoa yenye watoto kadhaa! 

Kwao hili hawakubaliani nalo. Lakini wakati huo huo kuna ambao walianza uhusiano wa kimapenzi kwa matatizo na hivi sasa bado wapo katika matatizo katika maisha yao ya kimapenzi.

Kwa ufafanuzi zaidi hebu soma visa vifuatavyo ambayo ni vya watu wawili tofauti, hapana shaka utakuwa na jipya la kujifunza. Mosi: Hiki kinamhusu Ben, alipokuwa anasoma Elimu ya Sekondari alitokea kumpenda sana Lucy na kwa bahati nzuri Lucy naye alikuwa akimpenda sana, wakawa katika uhusiano kwa misingi ya upendo na uaminifu. 

Wapenzi hawa walikuwa wakipendana sana na wakati wakianzisha uhusiano wao walikuwa kidato cha nne. Mpaka wanamaliza kidato cha sita hawakuwahi kukutana kimwili, baadaye kila mmoja akiwa anasoma chuo chake, walikutana nyumbani kwao Mbeya wakati wa likizo. 

Wikiendi moja wakaenda club, hiyo ndiyo ikawa siku yao ya kwanza kufanya mapenzi na wote wawili ilikuwa mara yao ya kwanza kushiriki katika sayari ya wapendao.

Siku zikaenda na walipomaliza chuo na kupata kazi wakaoana, wanaishi kwa furaha na amani, ingawa kuna matatizo madogo madogo ya hapa na pale ambayo huwa wanayamaliza wenyewe. Hivi sasa Ben ana miaka 38 na Lucy miaka 34 wana watoto wawili katika ndoa yao ya amani na mapenzi ya dhati.

Kisa cha pili kinamhusu Lilian; Huyu ni msichana, akiwa darasa la sita tayari alishaanza mambo ya mapenzi, mpaka anafika kidato cha tatu alikuwa kashatembea na wanaume zaidi ya ishirini! Hakufanikiwa kufanya mtihani wake wa mwisho wa kidato cha nne kwa sababu aligundulika ana ujauzito wiki chache kabla ya mtihani huo, mwisho wa masomo yake ukawa hapo.

Alivyojifungua akaanza kufanya kazi ya kuuza genge na kwa bahati mbaya mwanaye hakuwa na baba, maana hakujua mimba ni ya nani na kati ya wanaume watatu aliowashuku kuwa wanaweza kuwa ni mimba ya mmoja wao, alipowafuata walimfukuza kama mbwa.

Baadaye Lilian aliamua kutulia na kwa bahati nzuri akapata mpenzi mwingine ambaye alitulia naye akiamini anaweza kufuta machungu yake katika historia yake ya mapenzi, cha ajabu sasa baadaye akaachwa solemba. 

Akatafuta bwana mwingine akawa naye na kuachwa. Lilian sasa ana miaka 27 lakini ana watoto wanne na kila mmoja ana baba yake. Maisha yake siyo mazuri na chanzo kikubwa hapo ni mapenzi. Anajilaumu sana kujiingiza katika mapenzi ya utotoni. Maisha yake ni ya kubangaiza akiwa hana uhakika wa kupata mlo wa siku inayofuata.

Kwa leo kituo kikubwa kinakuwa hapa, wiki ijayo tutaendelea.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Secret Love. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake
 
Top