“Mimi tena niwe na mwanaume labda sio mimi… binafsi sitaki tena wanawake, wamewahi kunitesa sana,” ndivyo baadhi ya watu wanavyojisemea.
Hawa watu wengi wanaosema haya, ni wale ambao tayari walishateswa kwenye mapenzi, yawezekana ni mpenzi mmoja au hata zaidi.
Kwa nini watu wanateswa au kudanganywa katika mapenzi? Tafiti nyingi zinazohusiana na masuala ya mapenzi, ukiwemo ule wa mtaalamu kongwe katika tasnia hiyo, Robyn Carr alioupa jina la Newcomer, zinasema mara nyingi ukiona mtu anapata wapenzi wasiofaa, ni dalili pia yeye mwenyewe ana tatizo katika uchaguzi wake au uamuzi wake.
Kwa mfano, siyo sahihi sana mwanamke kukubali kuingia kwenye vitendo vya ndoa wakati bado hajaolewa.
Katika maeneo mengi unaweza kuona mwanamke analala na mwanaume kwa maana ya kufanya naye ngono, au hata kuishi kwake wakati mwanamume hajafuata taratibu za kindoa. Kuna haja gani ya kuhangaika kufuga ng’ombe ili uweze kupata maziwa, ikiwa sasa hujafuga na unapata maziwa utakavyo.
Mwanzo mbaya huzaa mabaya; Wanawake wengi wanakumbwa na matatizo kwa sababu wanayatafuta wenyewe. Kwa mfano kukubali kutumikishwa kama watu walioolewa kama vile kukubali kufanya ngono, wengine hadi wanalala na wanaume au hata kuhamia kwao, bila wanaume hao kufuata taratibu.
Mwanamke mwenye akili timamu hafanyi ya hovyo; Msomi wa kutoka Marekani, Lisa Jackson anasema katika chapisho lake la Tell me, yaani Niambie kwamba kutojitambua na kujithamini ndiko kunakowafanya wanawake wengi kuteseka katika mapenzi.

Anasema Lisa kwamba wanawake wengi ni mazumbukuku, ni watu wa kujikomba wala hawathamini utu wao. Wengine wanaomba ofa na kufikiri maisha kwao hayawezi kwenda bila kupewa ofa au zawadi kutoka kwa wanaume, ambao kwa bahati mbaya wengine wamekuwa ni wenye kuwapa mateso mno.
Wapo wanawake ambao wanajigonga kwa wanaume kwa kufanya nao ngono au hata kuhamia kwao kwa sababu tu wanahofia wasipofanya hivyo hawataweza kuolewa nao. Hata hivyo tafiti zinaonyesha kuwa wanaume walio makini, hupenda wanawake walio makini kwa kukataa kufanya ngono kabla ya ndoa au hata kukataa kulala nao kabla ya ndoa.
“Wanawake wengi hawalijui hilo, lakini ndiyo ukweli kwamba wanaume walio makini huoa haraka sana pale mwanamke anapompa masharti kwamba sitaki tufanye ngono, hiyo humpa faraha mwanamume kuona kwamba hakika huyu mwanamke hata nikimuoa itakuwa ngumu kwake kuchukuliwa na wanaume wengine kwa sababu hapendi kufanya uchafu (ngono),” anasema Lisa.
Ndiyo ukweli kwamba kama watu wamekuwa wakifanya ngono sana au kuwa na historia ndefu ya kufanya ngono kabla ya ndoa, maana yake ni kwamba hata wakioana, mmoja anaweza kubaki na hofu kwamba huenda mwenzi wake asiwe mwaminifu, maana hata yeye alimpata ndani ya muda mfupi. Wapo watu ambao anatongozwa asubuhi, mchana tayari wanafanya ngono.
 
Top