Ni kawaida katika mahusiano kuwa na magomvi yasiyokwisha juu
ya wapenzi kutoka nje ya mahusiano; si jambo la ajabu tena kwa maisha ya sasa
yaliyochanganyika tamaduni na historia mbalimbali.
Kama mwandishi na mdadisi wa maisha ya kila siku yamuhusuyo
mwanadamu, nimegundua sababu saba ambazo humfanya mwanamke ama mwanamme kukosa
uaminifu katika mahusiano.
Nimekuwa nikijiuliza kwa muda mrefu juu ya suala hili la
kukosa uaminifu katika mapenzi, kwa maana sikuona sababu ya msingi kwa mtu
kutoka nje ya mahusiano.
Kipi hasa kinachomfanya mtu akakosa uaminifu juu ya mpenzi
wake. Je ni starehe za kitandani? Ni starehe za maisha na raha za mahaba? Au ni
tama tu za kimwili..
Lakini waswahili husema utu uzima ni dawa, ingawa sijawa mtu
mzima wa hivyo kusema nimeona megi; ila maisha ya sasa hata watoto tunakutana
na misukosuko inayotulazimu kukua kabla ya umri kufika.
Nitaziainisha sababu hizo saba kwa maelezo ya kutosheleza,
ikibidi nitatoa mifano ya kusaidia kuelewa mada kwa utaratibi mzuri na
mpangilio mwema rahisi kuelewa.
Sababu ya kwanza: ni Kupungua mapenzi; hii imekuwa ni sababu
kuu ya kumfanya mtu atoke nje ya mahusiano. Kwani kawaida kuna watu hupenda
kudekezwa au kupewa mapenzi motomoto bila kupungua hata chembe kwa kipindi
chote cha mahusiano.
Kwa mfano; wakati penzi linapokuwa changa kuna kule
kupigiana simu kila dakika, mtaongea hata upuuzi na kuchekacheka huku
mkitaniana kama watoto wadogo. Ukila chakula fulani cha tunu utamwambia mpenzi
wako, wakati unapika ukijikata na kisu kwa bahati mbaya utampigia simu mpenzi
wako huku ukideka, na mengi kama hayo .
Mara nyingine mtatoka mandari (matembezi ya baharini au
jioni), mkiwa huko baharini mtarushiana maji, mtamwagiana michanga huku
mkikimbizana kwa vicheko.
Mara nyingine mnaweza kuwa mkahawani mkila ama mkinywa,
mpenzi wako anaweza kukulisha ama
akafanya kama anakulisha halafu anakwepesha au anakula yeye. Mradi tu mcheke
ama umpige kofi kidogo la mahaba, na stihizai za kilimbukei. Lakini hayo ndo
mambo ambayo wengi huwa nayo kwa kila penzi changa.
Baada ya kupita miaka miwili ama mitatu mambo kama hayo
hupungua. Hamtakuwa na muda tena wa kuchezacheza namna hiyo. Inawezekana kazi
zinawabana ama mwanamke anaweza kuwa amejifungua na mapenzi yote ameyahamishia
kwa mtoto.
Hapo sasa mume huanza kutafuta kibinti kidogo
kitakachomrudishia ile michezo ya awali aliyoizoea kutoka kwa mkewe. Unaweza
kumkuta mzee wa miaka hamsini lakini wakati akiongea na kimada wake wa miaka
ishirini huwezi kuamini, wanataniana na kuchekacheka kama mahantobwe au
mahayawani wa mapenzi.
Kadhalika mume anaweza kubanwa na kazi, mke kila akijitahidi
kupata nafasi ya kuchezacheza na mumewe huwekwa pembeni.
Anaweza kumpigia simu mumewe ofisini akaambiwa ana kazi
nyingi wataongea nyumbani, akitoka kazini jioni amechoka, akishawekewa maji ya
kuoga na kula huhamia mezani na ‘laptop’ yake anamalizia kazi za ofisini mpaka
usiku mwingi, akitoka hapo hujiagusha kitandani na kulala, asubuhi na mapema
kazini. Ikifika jumapili mama huanza kufurahia kwa kuona atakaa nyumbani na
mumewe, lakini baba atasema ana semina Bagamoyo na atalala hukohuko.
Hivyo, hayo ndiyo matatizo yanayomfanya mume au mke kuanza
kutafuta mtu atakaempa furaha kama zamani. Na ndiyo maana utakuta mume au mke
hayuko tayari kuharibu ndoa yake, ila hutoka nje ya ndoa. Kumbuka hajachoshwa
na ndoa, bali ni vitu fulanifulani tu anavikosa na ndivyo vinavyomfanya atoke
nje.
Sababu ya pili: ni
tamaa ya kupata zaidi ya akipatacho katika ndoa au penzi la kawaida tu
la uchumba.
Inaweza kuwa ni tamaa ya fedha au utundu wa kitandani,
husemwa mapenzi si fedha, lakini watu husahau kuwa mapenzi huendeshwa kwa
kutumia fedha.
Chukulia utataka kutoka mandari na mpenzi wako, lazima
mtahitaji kununua juisi, soda au chakula cha jioni kitakachowafanya muwe pamoja
usiku huo. Vilevile hata kama mpo katika ndoa, ni vema siku mojamoja muende
mkalale hotelini ili kubadilisha mazingira ili pendo lenu lizidi kushamiri.
Tazama mambo hayo
yote yanahitaji fedha, si za kumuhonga mpenzi wako la hasha, bali ni kugharamia
hayo matumizi ya kuimarisha pendo na kulipalilia furaha.
Ndiyo ukaona watu wengi huamua kutafuta wanaume au wanawake
watu wazima wenye kipato kizuri ili wapate fedha za kuja kufurahi na wapenzi
wao wanaolingana umri.
Na mara nyingine mwanume au mwanamke anaweza kuwa na mpenzi
mwenye fedha, ila bado anatoka nje; sababu huwa ni kutafuta ridhiko la
kitandani.
Zingatia hili: wanaume wengi hawawaridhishi wapenzi wao,
huwa na pupa ya kukimbilia tendo bila kumuandaa mpenzi wake. Matokeo ni
mwanamke kukaa katika mahusiano kwa miaka miwili lakini asiridhishwe
kimahaba na mpenzi wake. Hivyo huamua
kutafuta shababi mmoja atakaemtimizia haja yake.
Kumbuka mwaamke hajachoshwana ndoa, bali ni mambo fulani
fulani huyakosa; inawezekana anampenda mumewe kuliko hata huyu anaemridhisha,
lakini huamua kutoka nje ili aendelee kuwa na huyu mumewe wakati huohuo awe
anafurahia usichana wake. Sijui nimeeleweka hapa?
Ukitaka kugundua hili, mwanamke anaetoka nje ya ndoa akihisi
anagundulika yupo tayari kuachana na huyo anaeiba nae na si mumewe; sasa kama
ikiwa mumeo hakuridhishi si ubaki na huyu anaekuridhisha? Na si mwanamke tu,
hata mwanaume anaesaliti ndoa yake akihisi anagundulika haraka huachana na
hicho kibinti na kubaki na mkewe.
Ndoa zina mambo mengi, hilo ndilo jibu muafaka kwangu.
Unaweza kuwauliza wanawake mia moja juu ya mahusiano katika ndoa, na ukagundua
takriban wanawake thamanini hawaridhishwi na waume zao.
Kadhalika hata wanaume wapo ambao shughuli yao ni kubwa, kwa
wiki anaweza kumuingilia mke wake hata mara kumi. Kwa siku tendo moja anaweza
kufikia mshindo mizunguko mitatu mpaka minne. Sasa wanawake wengine ni dhaifu
huchoka haraka na mara nyingine huwakatalia waume zao.
Hivyo waume namna hiyo huamua kutoka nje ya ndoa na kutafuta
kahaba au janajike linaloweza shughuli anayoitaka yeye.
Haya si mambo ya kufikirika, ni vitendo ambavyo tunakutana
navyo katika jamii. Na ndiyo maisha ya kila siku ya mwanaadamu, si Afirika
pekee bali dunia nzima mambo haya yapo.
Kuna wanaadamu wa kipekee ambao hupendakufanya tendo kinyume
na maumbile. Hawa hufundishwa michezo hii na wapenzi wao wa kwanza kwa kuhofia
kupata mimba au kuharibu ubikira wao.
Sasa hufikia wakazoea michezo namna hiyo, pindi wakishaolewa
hupata bahati mbaya wakaolewa na waume wasiopendezewa na michezo hiyo ya kuenda
kinyume na maumbile. Hivyo hutafuta watu wenye kuipenda na hapo ndipo kutoka
nje ya ndoa kunapoanza.
Sababu ya tatu: ni kukosa wa kukujali; na mara nyingi sababu
hii huwahusu kina dada. Wanawake hupenda kujaliwa, ukimjali mwanamke na
kumsikiliza kilio chake hujisikia faraja sana.
Sasa, hutokea wakaolewa ama wakapata wanaume wakatili ambao
hawana muda wa kuwafuta machozi. Ndipo wanapotafuta wanaume wanaojua
kubembeleza huku wakifanya zaidi ya kubembelezana. Humpa mwili wake kama zawadi
ya kumjali.
Nitatoa mfano: mwanamke anaweza kuondoka nyumbani baada ya
kutaka kudekezwa halafu akagundua mumewe hana muda nae bali amekazana kuangalia
mpira au kuzungumza na marafiki zake huku wakinywa pombe.
Mke huamua kutoka nyumbani akatafuta mahala tulivu na kupata
kinywaji kuburudisha nafsi yake, au akaenda baharini kutuliza akili kwa upepo
mwanana wa bahari huku akitazama kupwa na kujaa kwa kurasa kuubwa nyeupe za
maji.
Huko anaweza kukutana na mwanaume ambae ni mchangamfu,
atamchekesha, atamtaniatania mwisho watakuwa marafiki na kuamua kumpa siri ya
moyo wake.
Zingatia hili, wanawake hawajui kuweka kitu moyoni, hudhani
akimpa kila mtu siri yake au tafrani zake ndiyo faraja asaa akapata msitiri wa kumliwaza. Na ndiyo
maana wanawake waliotendwa katika mahusiano niwepesi sana kutongozeka wakati
wakiwa katika kilio.
Mara nyingi wanaume wanaojua siri hizo za kinadada kwa lugha
ya kimombo huitwa ‘sharp shooters.’ Hawacheleweshi, hapohapo atampa bega lake
ili mwanamke apate pa kuegemea na kumaliza kilio chake.
Baada ya hapo wanaweza kupanga kukutana sehemu hiyo kila
siku au kila juma, na mabadiliko ya dunia kuna simu za viganjani, watakuwa
wanatumiana jumbe fupi za kuliwazana na kutakiana kheri ya usiku.
Mume ataona kero ya mkewe imepungua na kila siku ana furaha,
akiombwa ruhusa ya kutoka atafurahi kwani huona
atapata wasaa mzuri wa kukaa na marafiki wakitazama mpira, kumbe vyake
vinaliwa.
Kwa upande mwingine hata mume hupenda kujaliwa na kuonewa
wivu. Mke akijali sana watoto na mashoga akamsahau mume hilo ni kosa katika
mapenzi.
Kwa mfano, mume anaweza kuwa amerudi toka kazini amechoka,
mke amejitandaza upenuni anapiga soga na mashoga zake au ananyonyesha. Badala
ya kumuandalia mume maji ya kuoga au dunia ya sasa hakuna kuandaliana maji ya
kuoga, lakini japo ampokee mumewe mizigo, amsaidie kuvua nguo na kumkandakanda
mwili kutokana na siku nzito aliyokuwa ayo kazini, lakini hayo hayafanyiki.
Mume anapoona hapewi huduma hizo huamua kutafuta mtu mwenye
kuweza kutoa huduma hizo nae afaidi raha za dunia. Wewe utaona mumeo anatoka
kazini kila siku amechangamka, utaona amekupunguzia mzigo kumbe mwanamke
mwenzio anakusaidia.
Duniani kwa sasa huduma hizi hutolewa kama biashara, kuna
wanawake mahsusi wanawafanyia wanaume ‘massage’ na wanalipwa fedha nyingi.
Kifupi mwanaadamu hupenda kukandwakandwa mwili wake baada ya kufanya shughuli
ngumu ya kutumia nguvu au akili.
Sasa inapofikia wakati mwanaume anavua nguo ili akandwe na
jinsia ya kike tena si mkewe, sidhani kama hapo kuna usalama. Lakini ikiwa mke
atampa mumewe huduma hiyo ni salama zaidi katika kudumisha mahusiano.
Vilevile mume au mke anaweza kuwa na gubu au kelele kila
wakati; mara amembwatukia jirani, mara kamchapa mtoto, mara kamfokea mfanyakazi
za nyumbani. Alimuradi mume hana amani katika nyumba.
Akili yake imechoka anahitaji kupumzika au kufanya kazi zake
za ofisini nyumbani, matokeo yake huamua kutafuta sehemu kama baa au hoteli
iliyotulia ili afanye kazi zake huku anashushia kinywaji. Na baada ya hapo
anaweza kukutana na mijanajike inayosaka waume za watu na kuanza uhusiano. Mke
hapo inakuwa huna chako tena.
Sababu ya nne: ni mwanaume au mwanamke kutaka kutimiza ndoto
yake katika ujana. Tunafahamu vijana wanakuwa na ahadi nyingi, nyingine za
kipuuzi na nyingine za maana.
Sasa msichana ama mvulana anaweza kuweka ahadi ni lazima
atatembea na mtu fulani kimapenzi.
Mfano, binti anaweza kusoma shule moja na kijana ambae
alikuwa akimpenda kwa roho yake yote, ila alikuwa akiogopa kumwambia.
Hutokea miaka ikapita na wote wameshakuwa watu wazima, na
mara nyingine keshaolewa na kusahau hata hiyo ahadi aliyoweka.
Inatokea bahati tu siku anakweda kazini au sokoni akakutana
na huyo kijana, bado ni mzuri vilevile na mikogo yake ya shule na muonekano
vipo vilevile au vimezidi maradufu.
Hapo tena ile ahadi inamjia na pendo linaanza upya, husemwa
mtu mzima hana maya. Yaani watu wazima huambizana kiutu uzima. Si kama watoto
mpaka wazunguke, wajing’ate vidole au waanza kukunjakunja nguo.
Hapana, watu wazima wao huambiana kitu kilekile kilicho
moyoni. Hapo mapenzi huanza na labda kutokana na kumtamani siku nyingi mke
hugundua alikuwa akikosa vitamu kutoka kwa huyo kaka. Hapo tena balaa linaanza
la kutoka nje ya ndoa.
Hata mwanaume anaweza kuwemo katika kundi hilo la kuweka
ahadi kuwa mwanamke fulani ni lazima nimpate, lakini labda wakati anaweka ahadi
hiyo alikuwa kijana mdogo na hana pesa za kumghilibu au hana maneno matamu ya
kumhadaa.
Hivyo anapopata kazi na kuoa, mara nyingine nae alishamsahau
msichana huyo, wakikutana maofisini au njiani ndipo hukumbukana na kijana
huamua kutimiza ahadi yake, bila ya kujijua kuwa tayari yumo katika mkataba wa
ndoa na mwanamke mwengine.
Na wanaadamu wa siku hizi unaweza kumwambia nimeshaoa ama
nimeshaolewa na pete ya ndoa unayo, lakini bado hujisikia raha kufanya machafu
na wewe.
Sababu ya tano: ni kuficha udhaifu wako katika jamii
inayokuzunguka. Na hii inawahusu sana wakina baba.
Inaweza kutokea mwanaume ni mtanashati sana, awapo ofisini
au nyumbani huvaa nadhifu, afanyapo kazi zake huwa makini. Anapoijali familia
yake hataki mchezo; kifupi ni mfano wa kuigwa na shujaa.
Wanawake wengi hupenda wanaume mashujaa, wanaojali kazi na
familia zao bila ya kujisahau wao wenyewe. Maana wapo wanaume hujali kazi kiasi
hawakumbuki familia zao wala miili yao.
Hivyo kwa minajili ya kuwa shujaa katika jamii wanawake
wengi hutokea kujigonga kwa baba huyo; baba atajaribu kujiheshimu na kuamua
kuwakatalia, ima kwa wazi wakitumia neno ‘sitaki, nina familia’ au kwa kutumia
matendo tu; kama kutotimiza miadi ya mualiko wa chakula cha mchana au usiku.
Kukataa kahawa au maua anayoletewa ofisini na msichana huyo au hao.
Lakini jamii inayomzuguka baba huyo itaanza kudadisi
mienendo yake na wanawake hao. Maneno kama ‘anatupa bahati, au hana nguvu za
kiume ndo mana anakataa wanawake wazuriwazuri,’ yatakuwa mengi sana.
Na wanawake wakishasikia minongono kama hiyo ndipo
watakapozidisha vituko na kujionyesha wazi wazi kama mwanaume huyo haonyeshi
kuwajali ingawa wao ni wazuri na kila mwanaume angetamani kuwa nao.
Kama mwanaume huyo hatokuwa jasiri hapo sasa atataka kulinda
hadhi yake katika jamii na kuanza kusaliti ndoa yake. Huo huwa mwanzo wa kutoka
nje ya mahusiano.
Kadhalika hata mwanamke inaweza kumtokea hali namna hiyo;
anaweza kuwa ofisini bosi akawa anamtamani kimahaba. Atamuongeza mshahara,
atampa safari za kikazi ulaya na sehemu nzurinzuri. Lakini ataombwa mapenzi na
ahadi nyingi zaidi ya alivyopata ambavyo wafanyakazi wenzie hawana.
Atakapokataa kwa kutaka kulinda ndoa, wafanyakazi wenzie wa
kike wataanza kumuandama kwa maneno, ‘wewe huyo mumeo atakupa nini, unaacha
bahati kama hii, looohh shoga huna akili unaokota kopo la dhahabu mtaa wa kongo
unakataa kulichukua.’ Na maneno mengi namna hiyo.
Mwanamke ataona aibu kwa kutazama hali mbaya ya nyumbani,
mara nyingine labda ametishiwa kufutwa kazi na bosi kwa kukataa ombi lake ovu.
Hivyo huamua kusaliti ndoa yake si kwa kuwa hampendi mumewe, bali ni
kukabiliana na mitihani ya maisha iliyo migumu.
Sababu ya sita: ni msukumo kutoka kwa wazazi, mara nyingi
hii huwaathiri wanaume. Inafahamika sana wazazi hasa wa kike hupenda
kuwachagulia watoto wao wa kiume wake wa kuoa.
Na hii husababisha mikanganyiko ya mawazo kwa watoto wa wa
kiume mpaka kufikia kutoka nje ya ndoa ili kuwaridhisha mama zao. Kwani hali
huwa mbaya kiasi mama huamua kumtafutia mwanae wa kiume mwanamke mwengine ili
kumkomoa mkwe wake.
Sitoiongelea sana sababu hii, kwani inajulikana sana katika
jamii; kisaikolojia wazazi wa kike huwa na wivu sana kwa watoto wao wa kiume.
Hutamani wasiondoke nyumbani na ikiwa wataondoka basi waende kwa wake ambao
watawachagulia wao, na ikiwa hawajawachagulia basi wake watakaoolewa na wanaume
namna hiyo basi wajipange na mashambulizi toka kwa mama wakwe wao.
Mama anaweza kutafuta mtoto wa shoga yake na kumtambulisha kwa mwanae wa
kiume huku akijua tayari ni mume wa mtu; kinachotokea hapo ni urafiki wa kiwizi
au kihawara mradi tu amfurahishe mama yake.
Lakini ikumbukwe ndoa si kitu cha kukiteganisha hivihivi tu,
kwa maana labda wameshazaa, ama wameshakaa katika mahusiano kwa muda mrefu na
jamii imeshawazoea kuwaona hivyo. Kutengana na mkewe linakuwa jambo gumu lakini
ataamua kumfurahisha mama yake.
Kwa upande wa mwanamke inaweza kuwa tofauti kidogo, familia za kitajiri huwa hawapendi kuwaozesha
watoto wao kwa familia za kimaskini. Hivyo hutokea binti akalazimisha kuolewa
na mume anaemchagua, lakini katikati ya safari maisha yakawa magumu.
Anapoamua kurudi kwao, familia humtenga na kumwambia
‘tulikuonya usiolewe na huyo mume.’ Matokeo yake mwanamke huamua kutaka
kuwaridhisha wazazi wake kwa kutembea na mwanaume mwenye kipato, ingawa mume
wake wa awali hajaachana nae.
Maana hutokea ikawa ni ngumu kuachana nae kwani wameshazaa
na mara nyingine wameshazoeana.
Sababu ya saba: na ya mwisho kwangu si kwa kila mtu,
nasisitiza si kwa kila mtu kwa maana kila mtu atakuwa na sababu zake za kwanini
mtu anatoka nje ya ndoa. Sababu hiyo ya
saba inatoakna na kufufua penzi lililositishwa na hali ya maisha au mazingira.
Hapa nazungumzia utoto, fedha au jamii inayowazunguka
ilivyokua ikiwachukulia. Inawezekana mlipokuwa vijana mlikuwa katika penzi
motomoto, lakini kwa kuwa familia zenu zilikuwa na ugomvi wa muda mrefu hivyo
haikuwezekana kuoana, ama dini zilikinzana hivyo ukaamua kuoa au kuolewa na mtu
mwingine na kumsahau kabisa mtu Yule uliekuwa ukimpenda sana.
Lakini kwa muda fulani mlikosana na mwenza wako Yule wa
awali, ukakaa na mume au mke wako mpya hata kwa miaka kumi, ingawa ulikuwa
humpendi mume au mke huyo mpya lakini mmeshazaa na inawezekana umeshamsahau
mweza Yule wa awali.
Bila ya kutegemea unakuja kukutana na Yule mpenzi wako wa
zamani, ambae labda ndie aliekutoa ubikira au kama ni mwanaume ndie
aliekufungulia kitabu cha mapezi; kifupi ndie mpenzi wako wa kwanza kabisa
katika maisha yako.
Namna hiyo mara nyingi penzi huweza kuchipua upya bila ya
kujijua; ile nguvu ya penzi la dhati mlilokuwa nayo inaweza kuwafaya mkumbushie
ya zamani.
Kidogokidogo bila ya kujijua mnaweza kujikuta mnachipua
penzi lililolala siku nyingi kwani mlitenganishwa tu na mazingira na si ridhaa
yenu. Ni hatari sana kuoa au kuolewa na mtu ambae alilazimishwa kuachana na
mpenzi wake aliekuwa akimpenda kuliko chochote.
Hivyo sababu zote saba ni vema kuziangalia kwa makini na
kujiuliza wewe umeangukia wapi. Usilaumu wala kujilaumu ikiwa unaoa mpenzi wako
anatoka nje ya ndoa na kukosa uaminifu, ni vema kukaa nae chini kwa umakini na
kumuuliza sababu za kufanya hivyo; kukiwa na sababu za kuachana nae ni vema
kuachana kwa wema.
Nasema hivi kwa kuwa wapo watu ambao huwa katika ndoa ambazo
hawana furaha, bali hufanya hivyo kwa kuwa tu wana watoto, jamii inawasukuma au
familia ndiyo inayolazimisha watu hao kuwa katika ndoa.
Hivyo unapogundua mwenza wako amebadilisha mwenendo wake ni
vema mkakaa chini na kuzungumza kuhusu mustakabali wa ndoa yenu badala ya
kugombana bila ya kujua tatizo.
Kwa maana kuna mambo katika mahusiano huwa yanamalizwa kwa
mazungumzo na si kugombana, hili litasaidia kuepusha matatizo ya kiafya na
kiakili yanayoletwa na majuto baada ya talaka za kulazimisha.
Kwa hisani ya Hafidh Kido
Post a Comment
Kama umependezwa na hii stori toa maoni yako kama unayo