MAPENZI KWA NJIA
YA MDOMO, NI CHANZO KIKUU CHA SARATANI YA MDOMO NA KOO
Saratani
imeendelea kuwa tishio hapa nchini huku hofu ikiendelea kuikumba jamii kutokana
na wataalamu wa afya kushindwa kufahamu tiba halisi ya maradhi hayo hatari.
Takwimu kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road zinaonyesha ongezeko la
saratani ya mdomo na koo kwa kiasi kikubwa kutoka kesi 167 mwaka 2006 hadi 277
mwaka 2012.
Mkurugenzi wa
Idara ya Kinga
Ocean road, Julius
Mwaiselage anaeleza kuwa watanzania wasipende kuiga mambo ambayo si sahihi bila
kujua madhara yake kama kufanya mapenzi kwa njia ya mdomo. “Saratani ya mdomo
ipo, na nyingine zinasababishwa na zinaa “ anasema Dk Mwaiselage.
Tafiti za saratani
Tafiti mbalimbali
zimewahi kufanyika nchini na kubaini kuwepo kwa ongezeko la saratani ya
mdomo.Utafiti uliofanywa na Dk Innocent Mosha wa Kitengo cha Patholojia cha
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), umebaini aina za saratani 1,594, kati ya
hizo 509 zikiwa ni za midomo kwa mwaka 2003 pekee. Matokeo hayo yanaonyesha
kuwa kati ya saratani 509 za mdomo, saratani 242 zilisababishwa na Virusi vya
Human Papiloma ambavyo hutokana na zinaa. “Ninachojua mimi ni kuwa Virusi vya
HPV husababishwa na magonjwa ya zinaa, hivyo mtu anayeugua saratani ya aina
hiyo, imetokana na zinaa,” anasema Dk Mosha.
Wanaume waathirika
zaidi wa Saratani
Takwimu hizo ni
zile zilizopatikana kwa watu waliokwenda kufanyiwa uchunguzi katika Mkoa wa Dar
es Salaam pekee. Dk Mosha anasema kuwa wanaume ndiyo huathiriwa zaidi na
saratani ya mdomo ambapo kwa hapa nchini, asilimia 53 ya wanaume waliofika MNH
kwa ajili ya vipimo, walibainika kuugua saratani hiyo, huku wanawake wakiwa ni
asilimia 47. Utafiti kama huo ulifanywa pia na Dk Amos Mwakigonja, mkuu wa
Idara ya Patholojia katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili (MUHAS).
Dk Mwakigonja
alifanya utafiti wa saratani ya mdomo aina ya Kaposi’s Sarcoma ambapo wagonjwa
78 walibainika na saratani hiyo kuanzia mwaka 1990 hadi 2003. “Saratani za
mdomo zipo za aina nyingi na zimetofautiana kulingana na visababishi vyake,”
anasema Dk Mwakigonja. Katika utafiti wake Dk Mwakigonja alibaini kuwa wanawake
wengi walikuwa na saratani ya mdomo aina ya Kaposi’s Sarcoma kuliko wanaume.
Hata hivyo,
utafiti huo ulionyesha kuwa asilimia 50 ya wanaume walikuwa na saratani ya
mdomo hatari zaidi (systemic) kuliko wanawake ambao ni asilimia 37.
Mapenzi kwa mdomo
husababisha maradhi
Dk Mwakigonja
anasema kuwa mapenzi yoyote kwa njia ya mdomo lazima yasababishe maradhi ya
zinaa iwapo mmoja ameambukizwa. Pia anasema kwamba sampuli nyingi za wanaume
wanaojihusisha na mapenzi na wanaume wenzao (mashoga) zilibainika na saratani
ya mdomo. Utafiti huo ni sehemu ya utafiti wa Shahada ya Uzamivu ambao
ulionyesha kuwa wagonjwa wengi wa saratani ya mdomo walikuwa ni wanaume wenye
umri wa miaka kati ya 38 na kuendelea na wanawake ni 31.
Ufatiti wa WHO
Tanzania
Shirika la Afya
Duniani (WHO) pia lilifanya utafiti mwaka 2010 nchini kwa kushirikiana na Kituo
cha Taarifa za HPV, ambapo ilibainika kuwa asilimia 20 ya saratani za koo na
mdomo nchini zinasababishwa na ufanyaji wa mapenzi kwa njia ya mdomo.
Taarifa hizo za
WHO zinaeleza kuwa wanaume 747 hugundulika na saratani ya mdomo kila mwaka
wakati wanawake 472 hubainika na saratani hiyo pia. Wakati huohuo, wanaume
wanaopoteza maisha kutokana na saratani hiyo ni 444, kwa mwaka na wanawake ni
270, kwa mwaka. Utafiti wa WHO umebaini kuwa saratani ya mdomo inashika nafasi
ya sita katika aina 24 za saratani 24 zinazoisumbua zaidi Tanzania.
Ripoti hiyo
inaeleza kuwa wanaume wanaoathirika zaidi ni wenye umri wa kati ya miaka 15 na
55, ambao tayari wameshaanza kujihusisha na ngono. Kama maradhi mengine ya
kuambukiza, Virusi vya HPV huambukizwa kwa urahisi zaidi kutoka kwa wanawake
kwenda kwa wanaume kuliko kutoka kwa wanaume kwenda kwa wanawake. Utafiti huo
uliodhaminiwa na mfuko wa Bill na Melinda Gates na Kituo cha Saratani na Mpango
wa Utafiti wa Taasisi ya ICO unaeleza kuwa mitandao ya kijamii na picha za
ngono ndiyo chanzo cha watu wengi kuiga ufanyaji wa mapenzi ya aina hiyo.
Kwa mujibu wa
gazeti la The New York Times, tafiti zimefanyika na kubaini kuwa asilimia 70 ya
wagonjwa wanaobainika na saratani ya koo na mdomo duniani, husababishwa na
Virusi vya Human Pappiloma vinavyotokana na magonjwa ya zinaa.Tafiti hizo
zinaonyesha kuwa wagonjwa wengi wanaogundulika na saratani hiyo ni wanaume
wenye umri wa kati, wenye uwezo wa kifedha, wasiovuta sigara wala siyo walevi
waliokubuhu.
Utafiti huo
ulibaini kuwa wanaume wapo hatarini zaidi kupata saratani ya koo
inayosababishwa na Virusi vya HPV. Miaka ya 80, idadi ndogo ya watu waliougua
saratani ya koo walihusishwa na maambukizi ya Virusi vya HPV. Kihistoria, watu
waliobainika na ugonjwa huo, ni wenye umri wa miaka 70 kwenda juu ambao
walikuwa ni wale walevi waliokubuhu na wavuta sigara.
Ilielezwa kuwa
Virusi vya HPV vipo kwa wingi kiasi ambacho watu wazima wanaojihusisha na ngono
ya aina yeyote ile, huweza kupata maambukizi ya zinaa hata kama siyo saratani.
Hata hivyo ilibainishwa kuwa saratani isababishwayo na virusi vya HPV ni rahisi
kuitibu kuliko saratani ya koo isababishwayo na tumbaku au pombe kali.
Virusi vya HPV ni
nini?
Kwa jina la jumla,
saratani ya koo au mdomo huitwa saratani ya kichwa na shingo. (Neck and Head
Cancer) HPV ni miongoni mwa virusi hatari zaidi duniani visababishwavyo na
magonjwa ya zinaa na vinaweza kuathiri sehemu mbalimbali za mwili. Zipo aina
zaidi ya 120 za HPV, baadhi huweza kuzalisha usugu (warts) ambazo si saratani
katika sehemu za siri, mikononi na miguuni. Maambukizi ya HPV hufanyika kwa
urahisi, hata kwa kugusana ngozi au majimaji, huku maambukizi mengine
yakisababishwa na ngono.
Virusi hatari na
vinavyosababisha saratani ni HPV-16, HPV-18, HPV-31 na HPV 45. Aina hii ya
Virusi vya HPV husababisha saratani ambapo uvimbe waweza kujitokeza kwa ndani
na unaweza usionekane ukilinganisha na vivimbe vingine vya saratani. Wataalamu
wanasema HPV-16 na HPV-18 inahusishwa zaidi na saratani ya shingo ya kizazi na
endapo mapenzi kwa njia ya mdomo yatafanywa na mtu mwenye uambukizo huu ni rahisi
kuambukizwa.
Source:Nimeinyofoa
sehemu
Post a Comment
Kama umependezwa na hii stori toa maoni yako kama unayo