Mapenzi ni idadi kadhaa ya hisia zinazohusiana na mahaba, pendo na hata upendo wa Kimungu.Neno "kupenda" linaweza kurejelea aina za hisia, hali na mitazamo tofauti, kuanzia ridhaa ya jumla ("Napenda chakula hicho"), hadi mvuto mkali kati ya watu ( "Nampenda mume wangu"). Uanuwai wa matumizi na maana, pamoja na utata wa hisia zinazohusika, hufanya kuwe na ugumu katika ufafanuzi wa dhana hii, hata ikilinganishwa na hali zingine za kihisia.
 
Hisia
Hisiani mihemko ambayo binadamu na wanyama hujisikia moyoni na huathiri mwili pia kupitia ubongo.

Pendo
Pendo linaweza kutafsiriwa kwa maana mbalimbali, kama vile upendo, mapendo, mapenzi n.k.Hapa linatumika kwa maana ya ono mojawapo la msingi kwa binadamu na wanyama ambalo wanavutiwa na jambo fulani, hata likafuatwa na hamu na hatimaye furaha ikiwa jambo limepatikana kweli.Kati ya haja za msingi za nafsi, mojawapo ni kupenda na kupendwa.

Upendo
Upendo ni neno linalotumika kwa maana mbalimbali kuanzia hali ya nafsi hadi kwa Mungu. Linafanana na pendo, mapendo, mapenzi, n.k. Hapa linatumika kwa maana ya juu zaidi kulingana na Kigiriki "agape" na Kilatini "caritas".Katika teolojia ya Ukristo ni mojawapo kati ya maadili ya Kimungu, pamoja na imani na tumaini.

Kidhahania, mapenzi kwa kawaida yanarejelea hisia za ndani, zisizoelezeka, za kudumu kwa mtu mwingine. Hata hivyo, maelezo haya finyu pia yanashirikisha hisia tofauti, kutoka hamu na urafiki wa kimahaba na ukaribu wa kihisia wa kifamilia na kitaamuli, usiohusisha ngono  hadi umoja wa kina au ibada ya upendo] wa kidini.

Mapenzi katika aina zake mbalimbali husimamia mafungamano kati ya binadamu na, kutokana na umuhimu wake mkuu wa kisaikolojia, ni mojawapo ya maudhui yanayopatikana sana katika sanaa. 


Ufafanuzi
Neno la Kiingereza "love" linaweza kuwa na maana tofauti, lakini zinazohusiana, katika miktadha tofauti. Mara nyingi, lugha nyingine hutumia maneno mbalimbali kueleza baadhi ya dhana tofauti ambazo lugha ya Kiingereza hutumia neno "love" kurejelea; mfano mmoja ni wingi wa maneno ya Kigiriki yanayorejelea "mapendo". Tofauti za utamaduni katika kufafanua mapenzi hivyo, hufanya liwe jambo gumu kuanzisha ufafanuzi bia wowote.

Ingawa desturi au chanzo cha mapenzi ni suala ambalo hujadiliwa mara kwa mara, sura tofauti ya neno hili zinaweza kuwekwa wazi kwa kuamua ni nini ambacho sio mapenzi. Kama njia ya kawaida ya kuonyesha hisia chanya (aina kubwa ya kupenda), mapenzi kwa kawaida hulinganuliwa na chuki (au kutojali); kama upendo ambao umegemea zaidi kwenye uhusiano wa kirafiki kuliko wa kingono, mapenzi kwa kawaida hulinganuliwa na tamaa, na kama uhusiano kati ya watu, unaohusisha mahaba, mapenzi hulinganuliwa na urafiki, ingawa fdesturi zingine za neno mapenzi zinaweza kutumika kwa urafiki wa karibu katika miktadha fulani.

Wakati yanapojadiliwa katika hali dhahania, mapenzi kwa kawaida yanarejelea upendo kati ya watu, hisia alizo nazo mtu kuhusu mtu mwingine. Mapenzi mara nyingi yanahusisha kutunza au kujiainisha na mtu au kitu, ikiwa ni pamoja na nafsi ya mtu.

Aidha, katika tofauti za-kiutamaduni katika kuelewa mapenzi, mawazo kuhusu mapenzi pia yamebadilika sana na mpito wa wakati. Baadhi ya wanahistoria wanahusisha dhana za kisasa za mapenzi ya kimahaba na Ulaya wakati au baada ya enzi ya kati, ingawa kuwepo kwa mahusiano ya kimahaba kabla ya wakati huo kunaonyeshwa na ushairi wa kimapenzi wa kale.
 Mikono miwili ikiunganika kutengenezea umbo la moyo.

Kutokana na utata na udhahania wa mapenzi, mjadala juu ya mapenzi kwa kawaida hupunguzwa hadi maneno yaliyopitwa na wakati, na kuna mithali kadhaa kuhusu mapenzi, mojawapo ikiwa ile ya Vergilio ya kuwa "Pendo hushinda yote" na ile ya Beatles "All you need is love" (Unachohitaji ni mapenzi tu). 

Elimunafsia
(Elekezwa kutoka Saikolojia)
Elimunafsia (pia: saikolojia kutoka Kigiriki ψυχολογία psikhologia) ni fani ya elimu jamii inayolenga kujua nafsi ya binadamu ili kurahisisha ukomavu wake na uhusiano wake na wenzake.

Binadamu
Binadamu ni neno linalomaanisha "Mwana wa Adamu", anayeaminiwa na dini za Uyahudi, Ukristo na Uislamu kuwa ndiye mtu wa kwanza.

Ukomavu
Ukomavu wa binadamu ni hali iliyokusudiwa ifikiwe na mtu kupitia ukuaji wake.
Yaliyomo 
1.       Sifa za mtu aliyekomaa
2.        Pande mbalimbali za ukomavu wa mtu
3.        Mambo yanayozuia ukomavu
4.        Dalili za mtu asiyekomaa
Sifa za mtu aliyekomaa
1. Anayatambua mambo yalivyo. Anajitambua na kuwatambua wengine walivyo. Anatambua matukio pia katika sifa na kasoro. Anatambua yale anayoyaweza na yale asiyoyaweza. Hana wivu wala hofu. Anapima hali mbalimbali bila ya kufumba macho mbele ya mambo yasiyompendeza bali anatumia akili akabiliane nayo.

2. Anakubali hali ilivyo. Anajikubali na kuwakubali wengine walivyo. Akiona kasoro hachukii, bali kwanza anakubali hali ilivyo, halafu anajitahidi kuirekebisha iwezekanavyo. Hata akishindwa anakubali na kuvumilia. Vilevile anaweza kuyakubali mabadiliko na mambo mapya bila ya hofu, kwa kuwa anapima yote bila ya kufadhaika kwa kusema, “Itakuwaje?”

3. Anawajibika. Hangoji kuambiwa kila mara afanye nini na vipi, bali anaona mwenyewe anavyotakiwa kutenda, halafu anaamua kwa moyo ayatende. Ndiyo sifa kuu ya mtu aliyekomaa kweli: ana mwongozo wa maisha ndani mwake. Anazingatia pia kanuni za jamii na kusikiliza mashauri, lakini uamuzi wake unatoka ndani.

4 Anajiongoza kwa kuzingatia tunu alizojichagulia. Anaelekeza maisha yake upande fulani alivyoazimia. Katika kuamua la kufanya anafuata tunu hizo, si mkondo kama wanavyofanya kondoo.

5. Anahusiana vema na watu kwa sababu anawakubali, anawaheshimu na kuamini wanaweza kutenda mema. Anaelewa shida zao na kuwatimizia. Anawafanya wajisikie raha na kutokeza sifa zao. Mwenyewe anajisikia salama na kuwafanya washinde hofu zao na hivyo wakomae kwa urahisi zaidi.

6. Anafanikisha mipango. Ana mawazo ya kushangaza kwa kuwa mitazamo yake ni mipana na ya ndani zaidi. Mipango na miradi yake ni mingi, lakini haogopi kujaribu wala kushindwa, kwa kuwa anatambua mambo yalivyo na yanavyoweza kurekebishwa. Hivyo mara nyingi anafaulu kufanya mambo yawe alivyotaka. Mambo yaliyo magumu kwa wengine, kwake ni rahisi.

7. Anajiendeleza aishi kwa ukamilifu. Anatumia vizuri vipawa vyake vyote. Anafurahia mambo mbalimbali ya maisha na kufaidika nayo ili azidi kujiendeleza.

Pande mbalimbali za ukomavu wa mtu
1. Wa maono:
• anakubali maono yake bila ya kutawaliwa nayo; • anaweza kuyajulisha ili kusaidiwa; • anakabili magumu bila ya kuyaepa wala kuhangaika mno; • si mtu wa kujikinga kila mara.

2. Wa nafsi: • anasikiliza wengine, hatimaye anaamua mwenyewe bila ya wasiwasi mkubwa mno; • anaweza kubadili uamuzi wake akipata habari mpya; • anasema ukweli na kuchukua jukumu la uamuzi wake; • anapokea uamuzi wa watu  wengine.

3. Wa jamii: • anaona wema wa watu wengine, asijifanye lengo la yote; • anafungamana vema na wengine; • ana marafiki wa kufaa; • hawategemei mno ndugu zake; • anafuata taratibu za jumuia; • analinganisha mahitaji yake na ya kikundi chake; • yuko tayari kutimiza sheria halali hata zisipompendeza • anafanya kazi hata ngumu kwa utulivu.

4. Wa maadili: • anapokea mawazo mazuri na kuyaishi; • anafuata malengo yake kwa sababu anayo ya kufaa; • anatimiza busara, haki, nguvu na kiasi; • yuko imara katika imani, tumaini na upendo.

5. Wa roho: • anafungamana vema na Mungu, malaika na watakatifu; • anamtegemea Mungu na kutimiza matakwa yake; • anaelewa wito wake, anauthamini na kudumu kwa hiari kuuitikia.

Mambo yanayozuia ukomavu
Binadamu anakusudiwa kukomaa, lakini hafanikiwi sikuzote. Tunawaona watu waliolemaa upande wa mwili, lakini wengi zaidi wamelemaa upande wa nafsi. Sababu ni kwamba mtu akikosa haja zake za msingi hawezi kustawi. Haja hizo zina nguvu sana, nazo zisipotimizwa zinamuacha mtu kilema.Mambo yanayompata hata akalemaa kinafsi yanaelezwa na mviringo ufuatao usioelekea popote:

1. Hatimiziwi haja za nafsi, ambazo ni za msingi kama zile za mwili, hivyo zisipotimizwa yanaanza matatizo.

2. Hajisikii vizuri, hata kama ni mtoto au haelewi, kwa kuwa mtu akihisi hapendwi, hatakiwi, hayuko salama, basi anajisikia vibaya mpaka ndani.

3. Anapatwa na wasiwasi unaofanya nafsi isistawi, hata kama mwili unaendelea kukua. Ndiyo sababu anashindwa kushirikiana vizuri na watu au anajitenga nao kwa kuona hawampi anayoyahitaji.

4. Kutokana na hofu hashiriki vizuri katika mambo yote. Anatambua kwamba akibaki peke yake hapati nafasi ya kupendwa, lakini anashindwa kukabili hofu yake.

5. Matokeo yake ni kwamba anajihisi hastahili kutimiziwa haja zake. Hatimaye anaweza akajichukia kama kwamba ndiye anayesababisha watu wasimtimizie haja zake.

6. Anafadhaika asijue la kufanya mbele ya matatizo hayo. Anashindwa kupata jibu kuhusu haja zake kutimizwa kesho: ikiwa leo hapati anayoyahitaji hata kwa watu wenye wajibu kwake, je, atayapata lini?

7. Anafuata njia za kujikinga na hofu hizo kusudi asiendelee kufadhaika. Moja ya njia hizo ni kusukuma ndani kabisa mwa nafsi yake yale yasiyompendeza yasielee tena katika kumbukumbu; lakini kadiri mambo hayo yalivyoshindiliwa ndani yanamvuruga na kujitokeza kwa matendo na maneno yasiyotarajiwa. 

Njia nyingine ya kujikinga ni kutokubali hali halisi, yaani kukataa kukabili jambo la hatari au lisilopendeza. Njia nyingine ni kuhamisha dhihirisho la ono fulani (hasira, chuki n.k.) limlenge mtu tofauti na yule anayekusudiwa.

 Njia nyingine ni kuishi katika ndoto za mchana badala ya kuwazia hali halisi: mtu anajichorea akilini picha ya ulimwengu mwingine ambapo mambo yanakwenda anavyotaka, hata akaamini ndio wa kweli. 

Njia nyingine tena ni kujitafutia visingizio ili kutosikia aibu moyoni: mtu anaweza akafikia hatua ya kumshtaki mwenzake kwa kosa alilolifanya mwenyewe. Njia ya mwisho ni kudai kwamba wengine ndiyo wenye hali aliyonayo mwenyewe asiikubali.

8. Kwa kuwa njia hizo hazimtimizii haja zake, hazimsaidii ila zinamtuliza kijuujuu tu kwa muda, yaani zinafunika matatizo yake badala ya kuyatatua. Mtu amejikinga isivyofaa, basi shida inabaki palepale. Hivyo mviringo usioelekea popote umekamilika kwa kurudia namba moja: mtu anahitaji bado kupendwa, kukubaliwa, kuthaminiwa na kuwa salama. Nani atamsaidia?
Dalili za mtu asiyekomaa
1)      Anapurukusha tu na kulipua kazi mpaka asimamiwe.
2)      Hatimizi vizuri wajibu wake kwa jumla, ni mtegezi.
3)      Anachekacheka na kucheza wakati usiofaa.
4)      Ana kiburi cha kitoto.
5)      Hajui kujiheshimu wala kuwastahi wengine.
6)      Ni mbishi, pia kwa makusudi, tena mlalamishi.
7)      Hajui kulinda siri za nyumbani, ni mchongezi.
8)      Hajali maonyo, anayachukua kimzaha.
9)      Hakubali maoni ya wengine.
10)   Si mnyofu wala hajui kujieleza wazi alivyo.
11)   Anaogopa kutoa mawazo yake mbele ya watu.
12)   Haamui kwa utashi imara.
13)   Anafuata mkumbo.
14)   Katika kuwapenda wenzake ana ubaguzi.
15)   Anajipendekeza na kujipendea.
16)   Anadai kubembelezwa na kufarijiwa.
17)   Hana [[uvumilivu wala moyo mkuu.
18)   Anatunza kinyongo.
19)   Anakata tamaa kwa urahisi.
 
Top