Jambo hili limezua migongano mingi sana kwenye ndoa hadi kupelekea ndugu kuona kwamba mke au mume anamzuia ndugu yao kuwasaidia. Pia imeleta shida kwa wanandoa wenyewe kwa wenyewe. Tatizo mara nyingi sio ndugu bali ni wanandoa, mmoja anapoamua kutoa msaada kwa ndugu wa upande wake bila kumshirikisha mwenzie.
Mume na mke ni mwili mmoja, haijalishi nani anakipato
kikubwa, nani anafanya kazi au familia ipi inauhitaji mkubwa; haitakiwi na si
sawa kwa mwanandoa mmoja kuwasaidia ndugu wa upande wake kimya kimya. Hili ni
kosa ambalo limewagharimu wengi, mwenzio akigundua kuwa unasaidia ndugu zako
hata kama ni kidogo kiasi gani bila kumshirikisha hatafurahia, ataumia kwa nini
umemficha na atajiuliza ni mangapi mengine unamficha.
Usitoe chochote nje ya familia bila kumshirikisha mwenzi
wako, kabla hujaamua kumsaidia mshirikishe mwenzi wako na kwa pamoja muamue
msaada gani amtatoa na kwa kiwango gani na kwa muda gani. Pia kama mmeongea
ikaonekana hamna uwezo wa kutoa msaada kwa wakati huo, usiende kusema mimi
ningekusaidia lakini mwenzangu kakataa”,kwenye ndoa hakuna mimi na yeye bali
wote ni mmoja hivyo mweleze hali hairuhusu kwa wakati huo.
Pia usimkaribishe ndugu kuja kuishi nanyi bila kuongea
kwanza na mwenzi wako na mkakubaliana katika jambo hilo. Ni rahisi ndugu kusema
nanyanyasika kumbe mwanandoa mmoja amechukua maamuzi ya peke yake na hivyo huyu
aliyepuuzwa anamalizia machungu na hasira kwa ndugu aliyekuja. Matatizo mengi
katika ndoa yatamalizwa kwa ushirikishwaji wa kina kwa wanandoa wote na
kutokufanya jambo lolote bila kumshirikisha mwenzi wako.
Source: Women of Christ
Post a Comment
Kama umependezwa na hii stori toa maoni yako kama unayo