Mpenzi wako anayekupenda na kukuamini kupita kiasi, siku ukimtenda
ndivyo sivyo, atakaa na maswali mengi kwa muda mrefu. Utageuka kinyaa
mbele yake, kwa hiyo hata kukusamehe atapenda kufanya hivyo lakini
atachelewa kwa sababu heshima yako kwake, imeondoka kabisa.
Pili; mapenzi yenu ni kama mnalazimisha. Hampendani kabisa au yeye
hakutaki, kwa hiyo anaona hiyo ni fursa ya kukuadhibu. Utashangaa
umemkosea jambo dogo lakini anavyolisimamia utadhani umeua mtu. Kama
sura ya aina hiyo inajiri kwenye uhusiano wenu, jaribu kutazama mbele
kwa matumaini. Hakupendi, atakupotezea muda.
Tatu; mapenzi yake kwako ni ya wastani. Ulivyo kwake, ukiwa naye ni sawa
na hata usipokuwa naye, ni sawa vilevile. Huyu atakwambia anakupenda
muda mwingine kwa sababu anachukulia ni kauli ya mazoea. Ila
ukiyatafsiri mapenzi katika kipengele cha mguso wa moyo. Hakupendi, ila
amekuzoea.
Kwa mtu wa aina hiyo, mlipaswa kuwa marafiki lakini mkajidanganya mkawa
wapenzi. Hizo ni gharama za kulazimisha uhusiano. Elewa kwamba wapo watu
ambao inatakiwa uwe na urafiki nao wa kawaida, halafu yupo mmoja ambaye
ndiye mwenye nafasi yake. Anza kufanya upembuzi leo.
Mapenzi si kumuona mtu barabarani akakuvutia basi ukajiaminisha kuwa
huyo anakufaa. Mwenzi wa maisha yako ni lazima akidhi vigezo vingi. Wapo
ambao utalazimika kuwaacha barabarani wakirandaranda na dunia, halafu
yupo mmoja mahususi anayefaa kwa hali zote kuwa mwandani wako.
Mada hii ikupe tafsiri kwamba siku za mwanzoni za uhusiano wako, inafaa
utulize kichwa, ujadili mwenendo wa mwenzi wako kama anakufaa au la!
Uzuri wa umbo na sura yake, visikufanye uwe kipofu ukasahau kilicho na
faida kwa maisha yako ya leo na kesho. Tazama faida zaidi.
Unapoangalia tafsiri ya mwenzi wa maisha yako katika kipengele cha
bahati, ni vizuri ukaweka kando hisia za kuridhishwa kitandani. Ufundi
wake wa kukufanya usahau matatizo yako yote pindi mnapokutana faragha,
si lolote endapo hatakuwa na sifa za kutimiza matarajio yako ya
kimaisha.
Mwenzi wa maisha yako haendani na harufu yake. Kwamba ukiwa naye
unajisikia mtulivu kiasi gani, la hasha! Kinachobeba uzito ni kiasi gani
huyo uliyenaye anavyokupunguzia mzigo wa maisha yako. Je, mtindo wa
maisha yake, haukupi mzigo wa moyo? Kama jibu ni ndiyo, basi iwe heri.
Wengine hutafsiri kwamba mwenzi wa maisha yako utamtambua kwa namna
ambavyo anakufanya ujisikie hamu ya tendo mara kwa mara hata baada ya
kutoka naye faragha muda mfupi uliopita. Mtazamo huu nao ni potofu,
badala yake jiulize tena, je, mwenzi wako anakufanya ujihisi mtulivu?
Je, anakufanya ujione ni mwenye furaha? Nazungumzia furaha ambayo
inakuja yenyewe, siyo ile ya kulazimisha. Mwenzi sahihi kwako kwa zaidi
ya asilimia 99, anapaswa kuongeza kitu chanya kwenye maisha yako. Endapo
ukijitazama unajikuta unazidi kupotea badala ya kusafiri kwenye mstari
ulionyooka, hapo unazidi kupotea.
Yatazame maisha yako kabla hujakutana naye, halafu jiulize mabadiliko
yako. Je, ni hasi au chanya? Inawezekana kweli ameyafanya maisha yako
kuwa na furaha lakini hiyo furaha anaidumisha vipi? Isije ikawa
anakufurahisha pale tu anapokuwa na shida zake, pindi unapomtatulia huyo
anakwenda zake.