“Mimi tena niwe na mwanaume labda sio mimi… binafsi sitaki tena
wanawake, wamewahi kunitesa sana,” ndivyo baadhi ya watu wanavyojisemea.
Hawa watu wengi wanaosema haya, ni wale ambao tayari walishateswa kwenye mapenzi, yawezekana ni mpenzi mmoja au hata zaidi.
Kwa nini watu wanateswa au kudanganywa katika
mapenzi? Tafiti nyingi zinazohusiana na masuala ya mapenzi, ukiwemo ule
wa mtaalamu kongwe katika tasnia hiyo, Robyn Carr alioupa jina la
Newcomer, zinasema mara nyingi ukiona mtu anapata wapenzi wasiofaa, ni
dalili pia yeye mwenyewe ana tatizo katika uchaguzi wake au uamuzi wake.
Kwa mfano, siyo sahihi sana mwanamke kukubali kuingia kwenye vitendo vya ndoa wakati bado hajaolewa.
Katika maeneo mengi unaweza kuona mwanamke analala
na mwanaume kwa maana ya kufanya naye ngono, au hata kuishi kwake
wakati mwanamume hajafuata taratibu za kindoa. Kuna haja gani ya
kuhangaika kufuga ng’ombe ili uweze kupata maziwa, ikiwa sasa hujafuga
na unapata maziwa utakavyo.
Mwanzo mbaya huzaa mabaya; Wanawake wengi
wanakumbwa na matatizo kwa sababu wanayatafuta wenyewe. Kwa mfano
kukubali kutumikishwa kama watu walioolewa kama vile kukubali kufanya
ngono, wengine hadi wanalala na wanaume au hata kuhamia kwao, bila
wanaume hao kufuata taratibu.
Mwanamke mwenye akili timamu hafanyi ya hovyo;
Msomi wa kutoka Marekani, Lisa Jackson anasema katika chapisho lake la
Tell me, yaani Niambie kwamba kutojitambua na kujithamini ndiko
kunakowafanya wanawake wengi kuteseka katika mapenzi.
Anasema Lisa kwamba wanawake wengi ni mazumbukuku,
ni watu wa kujikomba wala hawathamini utu wao. Wengine wanaomba ofa na
kufikiri maisha kwao hayawezi kwenda bila kupewa ofa au zawadi kutoka
kwa wanaume, ambao kwa bahati mbaya wengine wamekuwa ni wenye kuwapa
mateso mno.
Wapo wanawake ambao wanajigonga kwa wanaume kwa
kufanya nao ngono au hata kuhamia kwao kwa sababu tu wanahofia
wasipofanya hivyo hawataweza kuolewa nao. Hata hivyo tafiti zinaonyesha
kuwa wanaume walio makini, hupenda wanawake walio makini kwa kukataa
kufanya ngono kabla ya ndoa au hata kukataa kulala nao kabla ya ndoa.
“Wanawake wengi hawalijui hilo, lakini ndiyo
ukweli kwamba wanaume walio makini huoa haraka sana pale mwanamke
anapompa masharti kwamba sitaki tufanye ngono, hiyo humpa faraha
mwanamume kuona kwamba hakika huyu mwanamke hata nikimuoa itakuwa ngumu
kwake kuchukuliwa na wanaume wengine kwa sababu hapendi kufanya uchafu
(ngono),” anasema Lisa.
Ndiyo ukweli kwamba kama watu wamekuwa wakifanya
ngono sana au kuwa na historia ndefu ya kufanya ngono kabla ya ndoa,
maana yake ni kwamba hata wakioana, mmoja anaweza kubaki na hofu kwamba
huenda mwenzi wake asiwe mwaminifu, maana hata yeye alimpata ndani ya
muda mfupi. Wapo watu ambao anatongozwa asubuhi, mchana tayari wanafanya
ngono.