Ifuatayo ni habari ya mwanamke ambaye aliwahi kuja kwangu kwa ushauri kuhusu ndoa yeke: Mama Kotilda Mkatah aliolewa mwaka 1980 na mume msomi aliyekuwa na wadhifa mkubwa kwenye taasisi moja ya fedha ya serikali.

Ndoa hii ilifungwa kwa sababu, Kotlida hakuwa na njia, lakini anasema, tangu wakiwa kwenye uchumba, alikuwa tayari na wasiwasi kama ndoa yao ingekuwa ni ya amani. Anasema, wakati bado wachumba, huyo bwana aliwahi kumpiga kibao kwenye kituo cha UDA kwa kosa la kuchelewa kufika kituoni kama walivyokuwa wamekubaliana.


Ndoa ilikuwa ni ya mateso makubwa hata kabla haijafungwa, Mwezi mmoja baada ya ndoa, mume alimwachia mkewe kazi kwa kwenda kufanya fujo ofisini kwa bosi wake kwa madai kuwa bosi huyo alikuwa na uhusiano na mkewe. Kotilda alianza kuishi kwa masharti. Hakuna kutoka, hata kwenda kwa jirani bila kuomba ruhusu na kutoa maelezo marefu kwa nini aende huko.


Kusimangwa, kukosolewa, kuitwa mjinga na mbumbumbu, ikaanza kuwa ni sehemu ya maisha ya mama huyu. Hali iliendelea hivi na kotilda akawa anajiambia, kuna siku hali itabadilika. Lakini, kwa bahati mbaya, hali haikubadilika. Wakati anakuja kwangu, alikuwa ameshaanza kuamini kwamba ni kweli alikuwa anastahili kutendewa vile na mumewe.


Huku ndiko tunakoita kufujwa. Mpenzi mmoja anapomuumiza mwingine kwa kauli zake au kimwili, mara kwa mara, tunasema hapo kuna kufujana.
Mpenzi mmoja anapokuwa na mamlaka aliyojipa dhidi ya uhuru na haki ya mwenzake, tunasema hapoimekuwa kufujana. mara nyingi, wanaofuja ni wanaume. Miongoni mwa matatizo ya ndoa ambayo mtu hashauriwi kuendelea kuyavumilia ni kufujwa. Ndoa ya kufujwa kuna maumivu makubwa ya hisia na mwili.


Ni vizuri hata hivyo, nikasema kwamba, neno kufuja ni mimi ambaye nimelibuni keelezea hali hii, ambapo mtu mwingine angeweza kuita mateso katika ndoa, kuonewa katika ndoa au kutumia istilahi yoyote.
Nimeipenda habari hii nikaona si mbaya nanyi wenzangu msome kwani tusinyimane elimu.
Chanzo: kitabu cha Mapenzi kuchipua na kunyauka na marehemu Munga Tehenan.
 
Top